Nabii na mchungaji wa kanisa la The God Church, Phronesis Ngwono amedai kwamba nchini Kenya, kanisa linapitia kipindi chenye changamoto nyingi mikononi mwa NEMA kuliko maeneo mengine.
Katika moja ya mahubiri yake katika kanisa lao lililopo Biashara Street jijini Nairobi, Ngwono alisema kwamba mamlaka ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira, NEMA imekuwa ikiweka vikwazo vikali dhidi ya kanisa hali ya kuwa maeneo kama misikiti licha ya kelele zao, bado wanaruhusiwa kuhudumu bila kudhibitiwa.
“Kuna upuzi unaoendelezwa na NEMA. Niliona baadhi ya maafisa wao wakiiwa kwenye kanisa, wanaingia mpaka kwa mimbari na kusema kanisa linapiga kelele. Na sijaona askari yeyote akiingia kwenye msikiti kusema wanapiga kelele. Na vipaza sauti vya kanisa vipo ndani hali ya kuwa vya msikiti vipo nje,” nabii huyo alisema.
Mchungaji huyo alimsuta rais Ruto kwa kutolitetea kanisa dhidi ya NEMA akisema kwamba yeye alikuwa anajitambulisha kama mwinjilisti kabla ya kuwa rais lakini baada ya kufikia ikuluni, ameliacha kanisa likitaabishwa.
“Rais Ruto unasema wewe ni mwinjilisti, lakini kanisa tunapiga kelele katika taifa lako! Sasa tunapiga kelele? Lakini hizi kelele zilikuwa nzuri kwako 2021 na 2022? Sasa watu wanaingia tu kwenye mimbari kipuuzi lakini kwa msikiti hawawezi enda,” alifoka.
Mchungaji huyo alisema kwamba imefikia hatua nchini Kenya kusajili kanisa ni mchakato mgumu kuliko kupata kibali cha kuuza vilevi.
“Sasa kanisa imekuwa kama eneo la kutupa taka na sehemu ya lawama, hatuwezi inua kichwa. Kusajili kanisa ni ngumu, afadhali uuze bangi. Kuuza chang’aa ni rahisi Kenya kuliko kufungua kanisa,” alisema.
“Kusajili kanisa Kenya ni ngumu, ni heri ukuwe mlanguzi wad aw za kulevya. Sheria na michakato mingi ambayo haina maana,” aliongeza kwa hasira.
Alimtaka waziri wa mazingira Aden Duale kama kweli anataka kufanya kazi yake ifaavyo, aanze kwa msikiti na kuamrisha spika zote kutolewa nje na kuwekwa ndani kama za makanisa.