Vincent Mboya amewashauri vijana wa Kenya walio katika tasnia ya burudani umuhimu wa kupanga kwa ajili ya siku zijazo
Akitumia mtandao wake wa Instagram, aliwauliza vijana ikiwa wamewahi jiuliza watakuwa wapi baada ya miaka kumi au kama bado watakuwa maarufu na tajiri watakapofikisha miaka 40.
“Ushauri wa haraka kwa vijana wa Kenya ambao wako katika tasnia ya burudani. Hivi sasa wewe ni maarufu na una mamia kadhaa ya maelfu au labda milioni moja au mbili kwenye akaunti yako, unaendesha gari nzuri na unaishi maisha mazuri."
"Sasa swali langu ni je umewahi kujiuliza utakuwa wapi miaka 10 ijayo? Je, bado utakuwa unaishi maisha hayo? Au hata ukifikisha miaka 40 bado utakuwa maarufu na tajiri?,” aliuliza.
Mboya aliendelea na kujibu swali lake na wakati uo huo akipeana ushauri kutumia uzoefu wake mwenyewe.
“Jibu ni hapana kwa sababu watu mashuhuri wengi wa Kenya hawafikirii kuhusu siku zijazo. Katika tasnia ya burudani ya Kenya, kuna kipindi ambacho unapata pesa nyingi, kisha ghafla kuisha,”
“Hili ni jambo ambalo nimejifunza na nimeamua kusaidia mmoja au wawili. Ikiwa una ushawishi sasa hivi, ushauri wangu kwako ni kutumia ushawishi huo sasa kukufanya uwe tajiri."
"Ikiwa ni kuacha sekta hiyo, basi uondoke na uanze kupata pesa halisi ambayo una hakika kuwa haitakauka kamwe. Watu watakucheka na kukukejeli kwamba ‘huyo ameisha’ lakini ni bora uishe sasa na unajua unachofanya,”
Anawashauri watu mashuhuri kutokuwa na haya na kufikiria jinsi ya kuzalisha mapato ya kweli hata kama ni kuajiriwa au kuanzisha biashara ili waweze kujitegemea.
“Fikiria jinsi ya kuzalisha mapato ya kweli. Anza biashara na ikuwe chini ya maji ama hata enda utafute kazi. Tumia ushawishi ulio nao kukusaidia kwenda hatua inayofuata maishani. Usiwe na haya! Acha burudani iwe kazi ya kando hata ikiwezekana pumzika na urudi baadaye,”
“Ninakuhakikishia kwamba mara tu unapoanza kupata pesa halisi, utafurahia kweli. Umaarufu huja na kupita huo ndio ukweli duniani kote lakini pesa itakuja na ni uamuzi wako kama unataka iende itaenda na huwezi kuiona tena,”