Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ametuma risala za rambirambi kwa familia ya marehemu mtayarishaji wa maudhui ya kidijitali, Tabitha Gatwiri.
Katika ujumbe huo wa heshima, Kalonzo alieleza kuwa kifo cha Gatwiri kilimwacha katika huzuni akimtaja kama mwanadada mahiri na mwenye ujuzi ambaye alikuwa ameazimia kufanya makubwa.
Musyoka akimuomboleza, alifichua baadhi ya mambo ambayo waliyajadili walipokutana miezi kadhaa nyuma.
“Moyo wangu unauma ninapoandika Ujumbe huu wa Rambirambi kwa familia ya Tabitha Gatwiri. Nilikutana na roho hii ya ajabu miaka michache nyuma. Gatwiri alikuwa mchangamfu kweli mwenye ujuzi."
"Alikuwa mwanamke mchanga aliyedhamiria kabisa kubadilisha ulimwengu kuwa bora na maoni yake. Majadiliano yetu kuhusu Hali ya Taifa na kile ambacho kizazi chake kingeweza kufikia, kikipewa fursa, yalikuwa ya kuchochea akili.”
“Majadiliano yetu ya mwisho yalilenga kuongeza utofauti wake kwenye Timu yangu ya Mawasiliano. Mwenyezi Mungu alikuwa na mpango tofauti kwa Gatwiri na njia yetu imebadilishwa kwa njia isiyoweza kurekebishwa,” alisema Kalonzo.
Kalonzo aliitakia familia yake subira na faraja wakati huu mgumu.
“Kwa familia ya Gatwiri, na Brian haswa, fahamu kuwa nina huzuni na kwa ajili yenu. Jua kwamba Gatwiri alikuwa nafsi incandescent; zawadi ya ajabu ambayo Mungu alituneemesha, hata kwa muda mfupi. Mungu wetu Mwenyezi anaye Gatwiri sasa. Amani ya Mungu, ipitayo akili zote, iwalinde mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu,” alimaliza.
Habari kuhusu kifo chake cha ghafla zilisambaa siku ya Alhamisi, Oktoba 31, 2024, baada ya mwili wake kugunduliwa nyumbani kwake.
Familia na marafiki zake walisema Gatwiri aliaga dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Mwili wa Gatwiri ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.