logo

NOW ON AIR

Listen in Live

“Kakangu alipofariki, niliishi kwa AirBnB peke yangu kwa siku 14 nikimuomboleza” – Eric Omondi

Akizungumza na Massawe Japanni kwenye kipindi ILIKUAJE, Eric Omondi alikiri kwamba kifo cha ndugu yake kilimuathiri pakubwa kwani si mtu ambaye alikuwa mgonjwa.

image
na MOSES SAGWEjournalist

Burudani03 November 2024 - 14:30

Muhtasari




Mchekeshaji aliyegeuka na kuwa mwanaharakati wa haki za kibinadamu, Eric Omondi amefunguka jinsi kifo cha ndugu yake mdogo kilimuathiri.

Fred Omondi, kaka yake mdogo alifariki mapema mwezi Juni baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani majira ya alfajiri.

Akizungumza na Massawe Japanni kwenye kipindi ILIKUAJE, Eric Omondi alikiri kwamba kifo cha ndugu yake kilimuathiri pakubwa kwani si mtu ambaye alikuwa mgonjwa.

“Mtu kama mimi bado haijaniingia kwamba ndugu yangu hayupo tena, naamka wakati mwingine tu na sijawahi kubali 100%. Ni afadhali upoteze mtu ambaye alikuwa mgonjwa pengine, umeenda kumuona hospitali… lakini hii ingine ya kutokea ghafla ni mbaya,” Omondi alisema.

Eric alifichua kwamba habari za kifo cha ghafla kwa mpendwa ni mbaya sana, akifichua kwamba dada yake mpaka leo hii miezi 4 baadae, hajawahi kuwa sawa.

Akielezea jinsi yeye amekuwa akijaribu kukubali kuwa kakake hayupo tena, Omondi alisema kwamba alimuomboleza Fred kwa siku 14 akiwa peke yake.

Alisema kwamba baada ya kuthibitisha kifo chake, alirudi kijijini kwao na kutaarifu familia na kisha akawakwepa. Aliingia katika jiji la Kisumu akakodisha chumba cha AirBnB na kujifungia kwa siku 14 peke yake ambapo alipata muda binafsi wa kumuomboleza Fred Omondi.

“Mimi nilitoka nikaenda nyumbani nikawataarifu na pale pia nikawahepa. Nikarudi Kisumu nikatafuta AirBnB na nilikaa hapo kwa siku 14. Nilirudi tu siku ya kuchukua mwili. Nilifanya hivyo ndio angalau nimuomboleze kaka yangu,’ alisema.

Eric alisema kwamba aligundua akiwa amezungukwa na watu kuna mambo mengi yanaendelea katika kichwa chake na ile siku wanaondoka ndio ukweli unaingia kwamba ako peke yake bila kaka yake.

“Nilisema safari hii nitakaa peke yangu nimuomboleze kaka yangu, nihisi kutokuwepo kwake na nikubali kwamba ni kweli Fred hayuko, kwa sababu awali iliniathiri sana kutokana na vifo vya wazazi wangu,’ alisema.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved