MFANYIBIASHARA Niffer ambaye ni rafiki wa karibu wa
msanii Alikiba ameripotiwa kutiwa mbaroni na jeshi la polisi Tanzania baada ya
kudaiwa kuchangisha pesa za kuwasaidia wahanga wa jengo lililoporomoka Kariakoo
sokoni.
Hii ni baada ya waziri mkuu wa Tanzania, Kassim
Majaliwa kutoa amri ya kukamatwa kwa mrembo huyo kwa kile alisema anachangisha
hela za msaada bila utaratibu mwafaka.
Majaliwa alitoa amri ya kukamatwa kwake wakati
alifanya ziara ya ghafla katika eneo la mkasa ambapo jengo la ghorofa 4
liliporomoka siku chache zilizopita.
“Yuko
binti ambaye anaitwa Niffer, mumeona anasema anachangisha na nimeona mpaka jana
alisema amekusanya zaidi ya milioni 37, atafutwe! Kwanza atuambie nani alimpa
kibali cha kuchangisha. Utaratibu huu wa kuingiza pesa kwa simu yake alipata
kibali wapi? Na amekusanya shilingi ngapi? Anasema ananunua maziwa, ameyapeleka
wapi?” Waziri mkuu alihoji.
Waziri mkuu huyo alithibitishiwa kwamba Niffer tayari
alikuwa amewekwa chini ya ulinzi na kuwataka kumhoji na kufunga ile akaunti
aliyokuwa akitumia kuchangisha pesa.
Kiongozi huyo pia alitumia kisa cha Niffer kama mfano
kutoa onyo kwa mwananchi yeyote wa taifa hilo dhidi ya kutumia fursa ya mkasa
wa kuporomoka kwa jengo la Kariakoo kuchangisha pesa bila idhini ya mamlaka
husika.
“Kwa
kuwa mmeshampata, mhoji na mhakikishe kwamba mmefunga ile akaunti. Na kupitia
tangazo hili, haturuhusu mtu yeyote kujitoa kusimamia michango ya watu kwa
ajili ya hapa,” Majaliwa alisema.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mikasa kama ule wa
Kariakoo upo chini ya wizara ya waziri mkuu, kitengo cha maafa. Katika kitengo
hicho, kuna sheria iliyopitishwa mwaka 2022 inayoratibu jinsi maafa kama hayo
yanashughulikiwa.
Wakili mmoja alieleza kwamba Niffer alifanya kosa
chini ya kifungu namba 36(2) cha sheria hiyo ya maafa ambacho kinasema kwamba
mtu yeyote atakayekusanya pesa za maafa bila kuwasilisha kwenye kamati ya
maafa, atakuwa amefanya kosa na adhabu yake ni kifungo cha kati ya mwaka mmoja
hadi miaka 5 jela au kulipa mara mbili ya fedha ambazo itabainika amezikusanya
au yote mawili.