KWA mara ya kwanza, msanii Diamond Platnumz
amefunguka kuhusu kukosa kuteuliwa kuwania tuzo katika kitengo chochote cha
tuzo kubwa za Sanaa duniani za Grammy.
Akizungumza na waandishi wa habari za burudani katika
kikao cha kuzindua kampeni ya chapa moja ya pombe nchini Tanzania, Diamond
alisema kwamba hapendi kuona mashabiki wake wakitoa kauli za kukata tamaa pindi
wanaposhindwa kukipata walichokuwa wakikitarajia.
Alisema kwamba siku zote katika maisha yake kwenye
muziki, yeye ni mtu anayeaminia sana katika kufanya kazi bila kujali ni nini
watu watasema huko nje.
Msanii huyo alifichua kwamba yeye baada ya kukosa
kuteuliwa kuwania Grammy, ilikuja kwake kama motisha ya kuachia ngoma kali hata
zaidi akilenga tuzo za mwaka ujao.
“La
kwanza mimi kama msanii jukumu mkubwa ni vkuhakikisha nafanya kazi iliyo bora
kuniingiza kwenye mashindano. Na kwenye mashindano pale ni lazima tukubali
kwamba si kila wakati wowote unaweza ukafanikiwa.”
“Na
tunapofeli kufanikiwa tusichukie, lazima tuongeze kasi na kuifanyia tathmini
kuangalia ni sehemu gani tuliteleza,” Diamond alisema.
‘Mimi
ni miongoni mwa watu tukikaa na timu yangu tusipochukua kitu chochote
hatujakipata. Wakianza kulalamika sipendi. Nawaambia pale huenda kuna sehemu
hatuko sawa. Pengine hatuna connection, au kuna dosari katika kazi yetu
tuliyoifanya,’ aliongeza..
Msanii huyo alimalizia akisema kwamba katika kila
kitu mtu yeyote anayefanya, matokeo yake lazima amuamini Mungu kwamba yeye
kapanga matokeo yawe jinsi yalivyotukia.
“Kwa
hiyo lazima ukubali kitu kinapotokea Mwenyezi Mungu ndiye kakipanga. Na kisikukatishe
tamaa ukaanza kutukana watu kwa sababu haya mambo yashapitwa na wakati. Jitathmini
mwenyewe, toa goma lingine na baadae mambo yatanyooka,”
alishauri.
Diamond alisema kwamba si yeye tu am baye alikosa
tuzo licha ya kufanya kazi nzuri, akisema wapo wasanii wengi tu kama yeye ambao
walikosa kuingia kwenye orodha ya Grammy.
“Kuna
watu wengi tu ambao hawakupata na walikuwa na kazi bora. Kwa hiyo sisi tuamini
tumefanya kazi iliyokuwa bora na tumepata mawazo mazuri ya kufungua dunia. Kwa sasa
hivi ni kumwaga mawe [nyimbo] mengi sana duniani. Mwenyezi Mungu atatuandikia
mwakani tunaingia [Grammy] na kama hatuingii tutafika kwa pamoja ama tunaungama
kwa sababu mimi naamini kwamba hakuna kisichowezekana,”
alimaliza.