Naibu rais aliyehenguliwa mamlakani Rigathi Gachagua amelalamikia asasi za usalama nchini kumhangaisha kwa kumfuata kila mahali anakokwenda wakitumia magari ambayo hayana nambari za usajili.
Gachagua amesema kwamba magari yasiyokuwa na usajili yamekuwa yakiegeshwa karibu na lango lake kwenye makao yake ya jijini Nairobi. Kwa mujibu wake, Gachagua amesema watu anaoamini kuwa maafisa wa usalama wanachunguza kila mgeni anayefika nyumbani kwake.
Vile vile, naibu rais huyo wa zamani amelalamikia kuwa maafisa hao wa usalama wanamfuata kila aendepo hadi nyumbani kwake kijijini katika kaunti ya Nyeri.
Gachagua amesimulia kisa ambapo kwa mujibu wake gari ndogo aina ya saloon lililokuwa limeegeshwa karibu na lango la nyumbani kwake, mnamo Jumapili lilimfuata hadi kanisa la PCEA Kerarapon. Gachagua amesema kwamba baada ya kuondoka kanisani hapo, gari hilo lilimfuata hadi sehemu amabyo alienda kula chamcha hadi aliporudi nyumbani kwake.
“Jumapili iliyopita, gari aina ya saloon lililokuwa limeegeshwa kwenye lango la makazi yangu lilinifuata hadi Kanisa la PCEA Kerarapon, lilinifuata nilipoenda kula chakula cha mchana na kurudi nyumbani!” Alisema Gachagua.
Kwenye taarifa yake, mbunge huyo wa zamani wa Mathira amesema kuwa uchunguzi wake ulionyesha kuwa nambari ya usajili wa gari lililokuwa likimfuata ilikuwa ya lori kwa mujibu wa mamlaka ya usafi na usalama barabarani NTSA.
Naibu rais huyo wa zamani aidha amesikitikia kuwa visa vya ufuatiliaji na kuangahishwa kwa wakenya kulishuhudiwa mara mwisho katika utawala wa miaka 24 wa aliyekuwa rais wa pili Daniel Arap Moi.
Hata hivyo, Gachagua amesema kuwa anahisi ni muhimu kuweka wazi visa vya kufuatwa na watu asiowajua hasa nyakati hizi ambapo visa vya mauaji ya kiholela vinashuhudiwa nchini.
“Katika enzi hii ya mauaji ya kiholela, utekaji nyara wa kulazimishwa na kutoweka na maajenti wa serikali, nimeona ni muhimu kushiriki na Wakenya unyanyasaji na vitisho ninaopitia, na kuwaarifu kuwajibisha serikali iwapo nitadhuriwa na maajenti wa serikali.” Alisema Gachagua kwenye ukurasa wake wa X.
Aidha aliomba
serikali iwachane nae akisema kuwa alitolewa ofisini na sasa ni raia wa
kawaida.
“Naomba serikali iniwache! Ulinifukuza ofisini, na sasa unapaswa kuniruhusu kururahia amani yangu kama raia.” Alisema Gachagua.
Madai ya Gachagua yanajiri siku chache baada ya idara ya DCI kupinga habari kuwa maafisa wake walitumia magari yasiyokuwa na usajili kujaribu kumzuia Gachagua kushiriki ibaada katika kanisa moja jijini Nairobi.