CASSYPOOL amefichua kwamba atakuwa katika kinyang’anyiro
cha ugavana wa kaunti ya Nairobi katika uchaguzi wa mwaka 2027.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Cassypool alisema
kwamba yeye haoni mshindani yeyote wa nguvu kando na gavana wa sasa Johnson
Sakaja na mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino.
Babu Owino amekuwa akitajwa kwa muda sasa kama mmoja
wa wanasiasa wanaopiga njaramba kujitosa kwenye dimba kuwania ugavana wa
Nairobi katika uchaguzi mkuu ujao.
Cassypool hata hivyo alionesha Imani yake ya
kuwabwaga wawili hao katika kile alichokitaja kuwa ni ‘mapema asubuhi’.
Hata hivyo, alipuuzilia mbali ushindani kutoka kwa
mtu mwingine yeyote, akimtaja msanii Bahati kama asiye na athari hata chembe
kwenye ushindani.
“Mimi
nasimama gavana Nairobi, saa kumi na mbili asubuhi nitakuwa nimemaliza hiyo
shughuli nimetandika kina Babu Owino, nimetandika Johnson Sakaja. Lakini Bahati
si mtu unahesabu katika mbio za ugavana, kwanza ni nani huyo anaitwa Bahati? Naongea
kuhusu Babu Owino atakayekuwa kwenye kinyang’anyiro, naongea kuhusu Sakaja. Watu
ambao nitatandika katika mbio za ugavana Nairobi,”
Cassypool alisisitiza.
Iwapo Bahati atakuwa kwenye kinyang’anyiro cha
ugavana Nairobi, basi haitakuwa mara yake ya kwanza kujitosa kwenye siasa.
Itakumbukwa msanii huyo aliwania ubunge wa Mathare
katika uchaguzi wa Agosti 2022 lakini akashindwa vibaya na kumaliza katika
nafasi ya 3 nyuma ya mshindi kutoka chama cha ODM na nambari mbili kutoka UDA.
Licha ya Cassypool kufichua kuwa atawania ugavana,
haibainiki kama anasema kweli ama ni moja ya mbinu zake za kutafuta kiki, kwani
amezoeleka na wengi kwa kauli ambazo mwisho wa siku huishia kutotekelezeka.