KIZAAZAA kilishuhudiwa katika ukumbi wa Polo jijini
Nairobi ambapo shoo ya Furaha Fest ilikuwa imeandaliwa usiku wa Jumamosi ya
Desemba 7.
Mashabiki wa Diamond Platnumz, mmoja kati ya wasanii
wakubwa waliotarajiwa kupakua burudani walibaki na nyuso zilizosawijika baada
yaq msanii huyo kukataa kutumbuiza.
Video ambayo ilionekana mahsusi na Radiojambo.co.ke
ilionyesha jinsi zogo lilizuka baina ya Diamond na umati wa mashabiki pindi tu
alipojitoma jukwaani.
Muda mfupi baada ya kuingia jukwaani, na hata kabla
hajaanza kupakua burudani kwa mashabiki waliofurika, Diamond alipata mapokezi
mchanganyiko, asilimia kubwa ya watu wakimfokea na kumnyoosea vidole.
Wengine walikuwa wanamfokea Diamond huku wakiimba
jina la msanii wa humu nchini, Willy Paul kwa mbwembwe, jambo lililompa
Diamond wakati mgumu kuendelea kutumbuiza.
Kwa ghadhabu, Simba – kama anavyojiita, aliondoka
stejini akiwa amekatishwa tamaa na hivyo ndivyo hakuweza kutumbuiza licha ya
mashabiki wengi kulipa gharama za juu kwa ajili ya kupata tumbuizo lake.
Inaarifiwa kwamba Diamond aliratibiwa kuwa wa mwisho
kutumbuiza lakini upande wake ulisisitiza atumbuize kabla ya Willy Paul ambaye
alikuwa atumbuize mwanzo.
Mfarakano huo ulisababisha ushindani wa kibabe baina
ya masabiki wengi wa Willy Paul na wachache wa Diamond Platnumz, kumpelekea
kuondoka ukumbini.
Hata hivyo, mpaka wakati wa kuchapishwa kwa ripoti
huu, upande wa Diamond haukuwa umetoa tarifa yoyote kuzungumzia tukio hilo.
Kwa upande mwingine, Willy Paul – ambaye anatajwa
kuwa miongoni mwa sababu za Diamond kusitisha tumbuizo lake ametoa taarifa
akisema kwamba alifanyiwa dhuluma katika hafla hiyo.
Pozee alihoji kwa nini Wakenya wanaruhusu kuonyeshwa
madharau nyumbani huku wageni wakionyeshwa heshima.
“Ninadhulumiwa
katika hafla hii, wanabadilisha ratiba dakika za mwisho, mbona Wakenya
wanakubali ili kutokea? Wasanii wa Tanzania wanapewa kipaumbele katika hafla
hii. Hii inasikitisha sana. Mbona Wakenya wanadharauliwa mbele ya Wabongo? Nitaendelea
kupigania bendera hii, nitaifia bendera hii,”
Pozee alisema huku akichapisha picha ya bendera ya Kenya.
Inasubiriwa kuonekana jinsi waandalizi wa Furaha Fest
watashughulikia malalamishiv haya, haswa kutoka kwa mashabiki ambao baadhi
wanahisi hawakupokea burudani jinsi walivyoptarajia baada ya Diamond kufeli
kutumbuiza.