MSANII wa kutoka humu nchini, Willy Paul amejitokeza
na kuzungumzia vitisho violivyorekodiwa na chawa wa Diamond Platnumz, Mwijaku
akimzomea kwamba hatomaliza mwaka huu na kuingia mwaka mpya salama.
Mwijaku, katika video ambayo imewagawanya watu
mitandaoni, alimpa onyo kali Willy Paul akimtabiria kupatwa na jambo baya baada
ya kuvurugana na Diamond wikendi iliyopita jijini Nairobi.
Mwijaku alimwambia Willy Paul kwamba kwa kumvuruga
Diamond hadi kumfanya kuondoka Kenya bila kutumbuiza, alifanya kosa lisiloweza
kusameheka.
Mbwatukaji huyo wa mitandaoni alifananisha kitendo
cha Willy Paul kumvuruga Diamond kama mwanamume kuingia choo cha kike, akisema
kwamba yatampata makubwa kabla mwaka huu kukamilika, zikiwa zimesalia takribani
siku 20.
“Willy
Paul, umeingia choo cha kike. Ukivuka huu mwaka kuingia 2025, labda mimi sio
Mwijaku,” chawa huyo wa Diamond alisema.
Hata hivyo, Pozee alionekana kutoyumbishwa na kauli
hiyo akisema kwamba bado azma lake ni kuendelea kupigania muziki wa Kenya,
liwalo na liwe.
Pia alisema kwamba atavuka mwaka 2025 salama na
ataendelea kuwepo hadi pale atakapoukomboa muziki wa Kenya kutoka mikononi mwa
mabepari.
“Wasanii
wa Kenya Wanastahili Heshima. Sasa hii ni nini? Hivyo kusimama Na Ukweli ni
Wrong Just Because Mtu Ni Mkenya? Nitamaliza mwaka Hadi 2025 Na Miaka mingine
Kwa Jina La Yesu. Kama nilivyosema, Nitapigania Nchi Yangu na Sekta ya Kenya
Hadi Tupate Heshima Tunayostahili,” Willy Paul alisema.
Kuvurugana na Willy Paul kulikuwa moja ya tukio kubwa
kutoka kwa Furaha Fest ambalo limekuwa likizungumziwa na watu kutoka matabaka
mbalimbali nchini Kenya na Tanzania.
Uvumi wa awali ulidai kwamba Diamond na Willy Paul
waliburuzana baada ya kutokea kutokuelewana kuhusu ni nani kati yao angefaa
kutumbuiza wa kwanza.
Hata hivyo, Diamond aliondoka katika hafla hiyo kwa
ghadhabu baada ya mashabiki kumfokea wakiimba jimba la Willy Paul.
Baadae, uongozi wake ulitoa taarifa ambapo walisema
kuwa Diamond kukosa kutumbuiza haikuwa kwa sababu ya Willy Paul bali ni suala
lililojiri baina yao na waandaaji wa hafla hiyo.