MSANII wa kizazi kipya nchini Kenya, Willy Paul
amefichua kwamba kipindi cha wiki moja iliyopita kimekuwa kipindi cha mavuno
makubwa kwa upande wake.
Pozee ambaye amekuwa midomoni mwa watu wengi tangu
usiku wa Desemba 7 wakati wa mfarakano ulioshuhudiwa katika tamasha la Furaha
Fest jijini Nairobi, amefichua kwamba akaunti zake za mitandao ya kijamii
zimeshiba pakubwa kwa kipindi hicho.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Willy Paul
alifichua kwamba amepata wafuasi wapya zaidi ya laki moja kwenye TikTok na
wengine wapya zaidi ya laki na nusu kwenye chaneli ya YouTube.
Msanii huyo zamani akiwa wa injili hakusita kutambua
kwamba hizo kwa asilimia kubwa ni juudi za mashabiki wake wa Kenya.
“Wakenya
Wamefanya. Tik Tok Yangu Imepata Wafuasi 100k Zaidi, YouTube Yangu Imevutia
Wafuatiliaji 150k Zaidi,” Willy Paul alifichua.
Willy Paul baada ya kufarakana na usimamizi wa
Diamond Platnumz katika tamasha la Furaha Fest lililoandaliwa katika Polo Club,
amekuwa katika mstari wa mbele kudai kwamba ndiye mpiganaji mkuu wa haki sawa
kati ya wasanii wa Kenya na wasanii wa kigeni.
Msanii huyo alidaiwa kuzushiana vurugu baada ya
ratiba ya kutumbuiza kwake kubadilishwa kinyemela, vurugu ambazo zilimfanya
Diamond kutopata nafasi ya kutumbuiza katika usiku huo wa tafrija.
Hata hivyo, baadae katika taarifa yake kwa njia ya
video, Diamond alikanusha kwamba kutotumbuiza kwake hakukuwa na uhusiano wowote
na Willy Paul bali ni wasimamizi walifeli katika kuhakikisha kuna utulivu.
Msanii huyo wa Bongo alifichua kwamba alilipwa zaidi
ya shilingi milioni 19 za Kenya na kudokeza kwamba asingerudisha hata senti
baada ya kutotumbuiza, kwani waandalizi ndio walienda kinyume na maagano ya
mkataba wa ujio wake.