WAKILI Ahmednasir Abdullahi ameomba msamaha wa dhati
kwa mashabiki wa klabu ya ligi kuu Uingereza, Arsenal baada ya kuitaka klabu
hiyo kumsaini mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford.
Siku chache zilizopita baada ya Rashford kutangaza
kwamba anahisi muda umefika kujaribu changamoto mpya mbali na Man Utd,
Ahmednasir alishauri kwamba huu ndio wakati mwafaka kwa Arsenal kuchangamkia
fursa hiyo.
Ahmednasir, shabiki kindakindaki wa Arsenal alisema
kwamba Arsenal wanafaa kuchukua fursa hiyo kwa haraka na kumleta Rashford ugani
Emirates.
“Arsenal
wanapaswa kumnunua Rashford katika dirisha la usajili la Januari,”
Ahmednasir aliandika kupitia ukurasa wake wa jukwaa la X.
Hata hivyo, alipokea maoni kinzani kutoka kwa
mashabiki wenzake jambo lililompelekea kufanya tathmini ya kina na kuibuka na
mtazamo mpya kuhusu Muingereza huyo mwenye umri wa miaka 27.
Wakili huyo alibaini kwamba Rashford huenda asiwe wa
umuhimu wa kipekee kwa Arsenal baada ya kupitia takwimu za uchezaji wake katika
klabu ya Man Utd.
Alifikia uamuzi kwamba Rashford ni mchezaji wa
kawaida tu kama wengine ambaye hawezi akaisaidia Arsenal katika mbio zao za
kusaka ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20.
Alitangaza kuomba msamaha mashabiki wenzake wa
Arsenal na kuondoa kauli hiyo ya kumtaka Rashford Arsenal.
“Misimu
10, mechi 439, mabao 139. Samahani, hiyo ni wastani sana. Ninaondoa kwa kuomba
msamaha, pendekezo langu,” Ahmednasir alisema.
Rashford amehusishwa kuondoka Man Utd haswa baada ya
kuachwa nje ya kikosi kilichomenyana na watani wao wa jadi Manchester City
wikendi iliyopita.
Hata hivyo, licha ya kumuacha nje ya kikosi, kocha
mkuu Ruben Amorim anasisitiza kwamba Rashford bado ni mchezaji wa Man Utd na
asingependa aondoke.
'Klabu ya aina hii inahitaji talanta kubwa na ana
talanta kubwa, kwa hivyo anahitaji tu kufanya kiwango cha juu na hiyo ndiyo
umakini wangu. Ninataka tu kumsaidia Marcus.
‘Hakuna kilichobadilika. Tunamwamini Marcus. Marcus
ni mchezaji wa Manchester United, kwa hiyo hakuna mabadiliko.’