RACHAEL Otuoma amevunja kimya kuhusu uvumi unaoenezwa kwamba huenda kuna matatizo ya kutoelewana baina yake na familia ya marehemu mume wake, Ezekiel Otuoma.
Akizungumza wakati wa
mazishi ya Ezekiel Otuoma Jumamosi katika kaunti ya Siaya, mrembo huyo alisema
kwamba watu hawakosi la kusema lakini kwake hawatoboi.
Rachael alionyesha
kwamba kuna uhusiano mzuri tu baina yake na familia ya marehemu mumewe, haswa
mama mkwe, mwanamke ambaye alimtaja kama nguzo muhimu katika maisha yake.
Rachael alisema kwamba
watu watasema huko nje na mwisho wa siku watalala, kwani yao wenyewe ndio
wanayajua hata kama watu wa nje wanajaribu kuingilia.
“Kwa mama mkwe, huyu
mwanamke ananipenda sana bwana. Mtasema hapo nje lakini mtalala. Za watu kwa
nyumba zao mtajaribu kunyoosha vidole lakini sisi wenyewe ndio tunajuana,”
Rachael alisema.
Aliahidi kutumia heshima
na taadhima ya marehemu mumewe kueneza upendo wake kwa mama mkwe.
“Mama mimi nakupenda
sana, na vile huyu mtoto wako alikuwa anakupenda, hivyo hivyo ndivyo na mimi
nitazidi kukupenda. Nitampa Otuoma heshima yake vile alikupa heshima yako na
vile alinipa heshima yangu,” Rachael alimwambia mama
mkwe wake.
Kabla ya Otuoma kufa,
kulikuwa na sekeseke kwamba mrembo huyo alikuwa na mtafaruku na wakwe zake,
jambo ambalo lilikuwa linazua mjaala mkali kwenye TikTok mara kwa mara.
Hata hivyo, Rachael
amesisitiza kwamba ni Amani tu kwenda mbele baina yake na wakwe zake, hata
akiahidi kwamba atadumisha upendo huo si tu kwa mama mkwe lakini pia kwa binti
wa Otuoma ambaye alizaa na mwanamke mwingine.
Mwanasoka huyo alizikwa
Jumamosi nyumbani kwao katika kaunti ya Siaya, takribani wiki tatu tangu
alipofariki.
Otuoma alifariki siku
chache kuelekea Krismasi mwaka jana baada ya miaka 4 ya mapambano dhidi ya
ugonjwa wa Motor Neurone – ugonjwa ambao wataalamu wa afya ya mwili wanauelezea
kama tatizo la kufifisha neva za mwili.
Alipatikana na ugonjwa
huo mwaka 2020 na mkewe Rachael amekuwa upande wake kwa kipindi chote haki kifo
chake, na alifichua kwamba huu ulikuwa mwaka wa kuadhimisha miaka 10 ya ndoa
yao.