PRISCILLA Ajoke Ojo, mrembo kutoka Nigeria ambaye ni mpenzi wa msanii Juma Jux kutoka Bongo amefunguka kwamba mwaka huu utakuwa wenye shughuli nyingi katika maisha yao ya kimapenzi.
Mrembo huyo amefichua kwamba huu ndio mwaka ambapo yeye na Juma Jux watafunga harusi rasmi na hata kufichua idadi ya watoto ambao atamzalia msanii huyo ambaye hana mtoto licha ya mafanikio makubwa kimuziki kwa miaka mingi.
Akizungumza na waandishi wa Habari katika uwanja wa ndege Tanzania Jumapili alasiri baada ya kutua, Priscilla Ojo alisema kwamba harusi yao itakuwa ya kipekee kwani itaoanisha tamaduni kutoka pande zote mbili – Tanzania na Nigeria.
“Huu mwaka tutaoana rasmi na Jux na harusi itafanyika kote; Tanzania na Nigeria.”
Mrembo huyo alipoulizwa ni nini kinamvutia kwa Jux kinyume na wanaume wengine haswa kutoka kwao Nigeria, Priscilla alisema kwamba msanii huyo ni mpole na mkarimu mwenye wingi wa mapenzi ya dhati.
“Jux ni mkarimu, mpole na ni mtu wa ajabu ambaye ni mkamilifu kwa kila sekta na pengine nitamzalia watoto 16 lakini tutaona idadi ya wale ambao Mungu atatubariki nao,” alijibu huku akisema tamanio lake ni kupata mtoto na msanii huyo wa ENJOY baada ya harusi.
Alisema kwamba familia yake nyumbani inamkubali Jux na inatamani kuona akidumu na Priscilla katika ndoa.
“Mama yangu anampenda, kila mtu nyumbani anampenda. Kumfahamu ni kumpenda tayari na mimi na yeye hatufikirii kama anaweza nisaliti kimapenzi,” Priscilla alisema.
Mrembo huyo aliingia katika uhusiano wa kimapenzi na Juma Jux mwaka jana na wiki chache baadae, msanii huyo akamvuta Diamond Platnumz studioni na kurekodi wimbo wa OLULUFEMI akimsifia Mnigeria huyo.
Jux, kama tu wasanii wengi wa Kibongo, hajakuwa na bahati ya kudumu kwenye uhusiano wa mapenzi kwani ameshuhudia huba lake likisambaratika mara si moja.
Lililoonekana kumuuma na kumsambaratisha zaidi ni kuvunjika kwa penzi lake na msanii Vanessa Mdee ambaye baadae alielekea Marekani na kuolewa na msanii Rotimi ambaye pamoja wana watoto 2.
Baadae, Jux alitia mkono katika kiza kinene cha mapenzi na kumvuta Karen Bujulu lakini penzi lao halikudumu kwani lilisambaratika mwaka jana siku chache kuelekea siku ya wapendanao ya Februari 14.