TIKTOKER Rachael Otuoma amefunguka hatua ambazo anataka kuzichukua ili kujiepusha na mawazo mengi kuhusu kufiwa na mumewe, mwanasoka Ezekiel Otuoma.
Kupitia mitandao wa
TikTok, mrembo huyo ambaye alimzika mumewe takribani wiki mbili zilizopita
alitangaza kwamba haijakuwa rahisi kuishi bila kipenzi cha moyo wake.
Rachael alisema kwamba
ameona akiendelea kukaa tu bure atajikuta amezama kwenye lindi la mawazo na
unyongovu, akisema kwamba sasa inambidi aanze kutafuta kazi za taaluma yake ya
kurembesha nyumba ndani.
Mrembo huyo pia alitangaza
kwamba anachukua likizo kutoka kwenye mitandao huo na kwenda kuzikata nywele
zake na wakati atakaporudi, kichwa chake kitakuwa na mfanano wa jinsi mumewe
alikuwa anapenda kunyoa.
“Naenda kunyoa, nikirudi
nitakaa Otuoma kabisa. Nataka kunyoa ule mtindo kama wa Otuoma. Mnaona ile
staili Otuoma alikuwa ananyoa halafu anaweka rugged hapa juu, hiyo. Unajua sasa
hivi mtu unafaa kufanya kile kitu ambacho kitakufanya ukuwe na furaha,”
Rachael alisema.
Kando na kunyoa, mrembo
huyo pia alisema yuko katika harakati za kutafuta makazi mapya na kuhama katika
ile nyumba ambamo walikuwa wanaiashi na marehemu Ezekiel Otuoma.
Rachael alisema licha ya
kuhama, hatouza au kupeana kiti ambacho Otuoma alikuwa anapenda kukalia kwa
nyumba, akiweka wazi kwamba mwishoni mwa mwezi huu atakuwa amefanikisha kuhama.
“Mawazo yataniua, kusema
ukweli nikikaa kwa nyumba tu hivi kila wakati nafikiria sana. Nikipiga kona
hivi naona picha ya Otuoma ikinitabasamia, huku kwingine naona Otuoma na mimi
vile alikuwa anatabasamu kwa kile kiti chake pale. Hiki kiti sitapeana, nataka
tu kutafuta kazi niwe busy.”
“Jumatano niko na kazi
moja na lazima nitaenda kwa sababu kukaa tu hivi mawazo yataniua. Nitakufa na
stress. Kuhama nitahama hivi karibuni, mwishoni mwa mwezi huu. Nitatoka hapa,” Rachael
alisisitiza.
Mwanasoka huyo alifariki
mwishoni mwa mwaka jana, siku chache tu kuelekea sikukuu ya Krismasi na kuzikwa
wiki ya kwanza ya Januari mwaka huu.
Kabla ya kifo chake,
Otuoma alipigana vita dhidi ya ugonjwa wa Motor Neurone ambao unaathiri neva za
mwili kwa kipindi cha miaka4 tangia mwaka 2020.