ALIYEKUWA msanii wa lebo ya Bahati, EMB Records, Weezdom amekuwa mtu wa kwanza kukosoa vikali kolabo mbili za Bahati na Willy Paul zilizoachiliwa Ijumaa Januari 31.
Kupitia ukurasa
wake wa Instagram, Weezdom alidai kwamba kolabo hizo mbili – Keki na Paah, hazikuwa
na ubora wowote licha ya Bahati na Willy Paul kuzipigia debe pakubwa.
Weezdom
alisema kwamba alijutia kutumia muda wake kusikiliza tungo za wawili hao ambao
waliondoka katika fani ya miziki ya Injili, akiwataka warudi kwenye injili.
Msanii huyo
ambaye pia alionekana kupotoka kutoka kwa injili kuwafuata wawili hao
aliashiria kwamba yeye bado ni msanii wa injili na kusema yuko tayari
kuwakaribisha wawili hao watakapofikia uamuzi wa kurudi.
Kwa mujibu
wa Weezdom, Bahati na Willy Paul wakirudi kwa fani ya miziki ya injili angalau
wataonewa huruma, akidai kwamba fani ya miziki ya kidunia imewakataa na ngoma
zao haziwezi onewa huruma hata chembe.
“Ni
nini hiki ambacho nimekisikiliza? Wuueh, kusema ukweli kila mtu ako na maskio
yake. Lakini aai, hapo hakuna kitu. Watu watafute watu wa kuandika ngoma kusema
kweli, ama mrudi kwa injili yetu hapa angalau huku kuna huruma mtahurumiwa,” Weezdom aliwaasa.
Kuelekea muda
wa kuachiliwa kwa kolabo hizo, Bahati alidai kwamba hii ni enzi mpya ambayo
yeye na Pozee wameanza, akisema kwamba wamekuwa wakitawala muziki wa Kenya kwa
miaka 10 iliyopita na sasa hawako tayari kuondoka.
Msanii huyo
alidai kwamba msanii yeyote ambaye hakuchukua fursa ya kufaidika kutokana na ugomvi
wake na Willy Paul basi atakufa maskini kwani bifu lenyewe tayari limefika mwisho.
“Unajua sasa hivi ndio tumeanza, ni enzi mpya na
ujue bado sisi ndio tumekuwa tukishikilia kwa miaka 10 na ndio tunaanza tena.
Hivyo kama kuna msanii hakutengeneza pesa huo wakati ajue sasa atakufa maskini
maana sisi tumerudi,” Bahati alisema huku Willy Paul akimuunga mkono kwamba hii ni enzi ya
kuwafuuza wasanii wa kigeni kutoka kilele cha chati za muziki humu nchini.