MENEJA wa Bradey Mtall maarufu kama Gen Z Goliath, Director Trevor ametoa kauli yake kuhusu video inayopiga misele kwenye mitandao ya kijamii ya jamaa huyo wakati wa ziara yake jijini Dubai, UAE.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Trevor
alikashifu video inayomuonyesha Bradley akishrutishwa kucheza karibu na simba
jike.
Bradley Mtall amekuwa Dubai kwa wiki
moja, shukrani kwa kampuni ya Zam Zam ambayo inajishughulisha na uuzaji wa
bidhaa za kielektroniki haswa simu za iPhone.
Trevor ambaye hivi majuzi ameweka wazi
kwamba Bradley alipata meneja mpya wa kusimamia shughuli zake zingine na
kumuacha Trevor kama meneja mbadala, hata hivyo aliwashukuru Zam Zam kwa kile
wanachomfanyia Bradley.
Trevor alisema kwamba licha ya Zam
Zam kumsaidia Bradley, haifai kabisa kumshurutisha kucheza karibu na mnyama
mwitu hatari kama simba hata kama amefungwa.
“Nimekutana na video inayoenea
ya Goliath na Zam Zam, na ningependa kuchukua muda kidogo kukashifu vikali
maudhui kama yale. Wakati ninahongera sana juhudi za Zam Zam kumpa sapoti Gen Z
Goliath wetu, ni vizuri kuelewa kwamba ubunifu una mipaka yake,”
Trevor alianza.
Trevor aliwataka Gen Goliath na Zam
Zam kwa Pamoja kuondoa mara moja video hiyo ambayo imekuwa gumzo kwenye mtandao
wa TikTok.
Trevor pia alibainisha kwamba video
hizo zinachapishwa bila uhakiki kutoka upande wake kama meneja.
“Ningependa kwa heshima kubwa
kuwauliza wafute video hiyo ya TikTok ambayo imekuwa ikipiga misele mitandaoni.
Pia ningependa Wakenya wajue kwamba video hizi zinachapishwa bila sisi
kuidhinisha kwa sababu hatuna haki kwazo.”
“Mwishow a siku, utengenezaji
wa maudhui ni safari ya kujifunza. Wakati mwingine, tunafanya makosa bila
kugundua, lakini cha muhimu ni kwamba tunatambua makosa hayo na kujifunza
kutokana nayo. Ningependa kuwajulisha kwamba makosa kama hayo hayatatokea tena
mbeleni,” Trevor alisema.
Video ya Bradley Mtall akicheza na
simba jike jijini Dubai imekuwa ikisutwa na wengi, baadhi hata wakizua utani
kwamba simba huyo akifanya makosa kumpararua kijana huyo basi wote watajitokeza
na kufurika jijini Dubai wakitaka haki kutendeka.