MUTHONI Truphena, mrembo wa KENYA mwenye umri wa miaka 21 amewakaribisha Wakenya wote kushuhudia mchakato wake wa akilenga kuweka rekodi mpya ya dunia ya kukumbatia mti kwa saa 48 mfululizo.
Truphena, ambaye kupitia ukurasa wake
wa Facebook anajitambulisha kama msanii na mwanaharakati wa masuala ya afya ya
kiakili alisema analenga kuweka rekodi hiyo kwa kuitengua ile inayoshikiliwa na
raia kutoka Ghana, Hakim Abdul.
“Leo ni siku ya hesabu. Kuanzia saa
kumi na mbili jioni kwa saa za Kenya, nitaanza changamoto yangu ya kujaribu
kukumbatia mti kwa saa 48 na kuzidisha rekodi ya sasa ya saa 24,” alisema
Muthoni.
Mrembo huyo aliwakaribisha Wakenya
wote kujitokeza kushuhudia akiweka rekodi hiyo ya dunia kwenye kitabu cha
Guiness katika bustani ya Michuki.
Kulingana naye, uchaguzi wa Michuki
Park ni wa kimkakati kwa sababu msukumo wake ulitoka kwa Waziri wa Mazingira wa
wakati huo John Michuki ambaye alichangia pakubwa katika kubadilisha Mbuga hiyo
na Mto Nairobi.
Bustani ya Michuki, ambayo zamani
ilijulikana kama Mazingira Park, iko kando ya Mto Nairobi kutoka Globe
Roundabout hadi Daraja la Makumbusho na ina upana wa eneo la takriban hekta
10.4.
Kwa mujibu wa jarida la People Daily,
nia yake inalenga kutoa ufahamu juu ya umuhimu wa Asili katika kupambana na
maswala ya afya ya akili ambayo anayataja kama janga nchini.
"Maswala ya afya ya akili
yanaleta shida kati ya vijana na umma kwa ujumla, kwa bahati mbaya, watu
hawathamini nguvu ya Mama Asili ya uponyaji. Ikiwa una msongo wa mawazo, tembea
tu katika bustani ya jirani na ukute mti au ukae chini ya mti,”
alinukuliwa na gazeti hilo.
Ili kufikia kuweka rekodi mpya,
Muthoni amekuwa akifanya mazoezi kwa takriban miezi 5.
"Nimekuwa nikitembea kwa
muda mrefu kila asubuhi na jioni kwa wastani wa kilomita 42, hii imesaidia
katika kuimarisha misuli yangu,"
aliongeza.
Pia amemshirikisha kocha wa yoga kwa
ajili ya kujitayarisha kiakili.