SIKU moja baada ya kuachia kolabo zao mbili, Willy Paul na Bahati sasa wamedadavua kiasi cha pesa ambacho video ya ngoma moja – Keki, iligharimu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram,
Willy Paul alifichua kwamba video ya ngoma hiyo ambayo imewavutia wengi chini
ya saa 24 baada ya kuiachia ilimgharimu Zaidi ya shilingi milioni 3 pesa za
Kenya.
“Nilitumia taslimu ya Shilingi
milioni 3.5 kwenye video hii na ndugu yangu Bahati. Bahati sasa yuko kwenye
mikono salama,” Willy Paul aliandika.
Bahati alifika kwenye chapisho hilo
na kumtania Willy Paul akimtaja kama “msanii Tajiri”.
Hata hivyo, licha ya ngoma zao
kuwavutia wengi, baadhi wanahisi kwamba hazijafika viwango ambavyo wengi
walitarajia.
Mmoja wa wanaokosoa ngoma hizo ni
msanii Weezdom ambaye alidai kwamba hazina ubora wowote akionekana kujuta
kuyapa masikio yake nafasi ya kuzisikiliza.
Kwa mujibu wa Weezdom, Wawili hao
wanastahili kutafuta watu wa kuwatungia nyimbo wao wasalie tu katika kuimba,
akikashifu utunzi wao.
Weezdom aliwasuta akiwataka kufanya
hima kurudi katika Sanaa ya injili, akidai kwamba huko angalau wataonewa
huruma.
“Ni nini hiki ambacho
nimekisikiliza? Wuueh, kusema ukweli kila mtu ako na maskio yake. Lakini aai,
hapo hakuna kitu. Watu watafute watu wa kuandika ngoma kusema kweli, ama mrudi
kwa injili yetu hapa angalau huku kuna huruma mtahurumiwa,” Weezdom aliwarai.
Itakumbukwa
kwamba Weezdom ni msanii aliyechipukia kimuziki shukrani kwa Bahati na lebo
yake ya EMB Records.
Hata
hivyo baada ya Bahati kuhamia miziki ya kidunia, ukuruba wake na Weezdom
ulionekana kuzorota ambapo msanii huyo amekuwa akimzomea hadharani mitandaoni
bosi wake wa zamani.
Mwaka
jana pia Weezdom alimkasifu Willy Paul kwa kile alidai kwamba alikataa
kujitokeza kumpa msaada wakati alikuwa amelazwa hospitalini.
Weezdom
alifichua kuzuiliwa katika hospitali moja kwa Zaidi ya miezi 3 katika kile
alichodai kwamba ni kukosa bili ya matibabu.
Alirudi
kwa mashabiki wake wa mitandaoni na baada ya kufanikiwa kutoka, alisema kwamba
illy Paul alifumbia jicho suala lake la uhitaji wa msaada kulipia matibabu
yake.