
MSANII wa miziki ya kizazi kipya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Prince Nemiala maarufu kama Ya Levis ameendelea kubadilisha dhana ya muziki kutoka taifa hilo kuwa ni Rhumba na Lingala tu kwa nyimbo zake za kipekee.
Ya Levis ambaye ameibuka kuwa jina maarufu miongoni mwa
wasanii tajika katika ukanda wa Afrika Mashariki amekuja na mtindo wa ngoma za
kutoka DRC – ambazo si Rhumba na zimepata mapokezi mazuri katika miaka ya hivi
karibuni.
Baada ya kuwapunga wapenzi wa muziki mzuri na nyimbo zake
kama ‘Mbangu Te’, ‘Libala’, ‘Nakati’ miongoni mwa nyingine, msanii huyo sasa
amerudi na wimbo mwingine kwa jina ‘Katalay’.
Akizungumza wakati wa kuupigia debe wimbo huo, Ya Levis
alifichua maana ya kina ya wimbo huo wenye mchanganyiko wa ladha ya R&B na
Afro-pop.
“Wimbo huu unahusu kukumbatia mapenzi bila kusita. Ni juu ya kuachilia
na kujisalimisha kwa hisia ambazo hutufanya tujisikie hai,” anasema Ya
Levis.
Ni wimbo ambao ameutoa katika majira sahihi wakati ambapo watu wanasherehekea mapenzi, ukiwa na mdundo taratibu wenye wingi wa ladha ya mahaba.
Ujio wa Ya Levis katika tasnia ya muziki wa Kenya
ulifahamika zaidi na wimbo wake wa ‘Nakati’ aliouachia miaka minne iliyopita,
wimbo ambao uliibukia kuwavutia mashabiki wengi wa muziki.
Nyota huyo mwenye vipaji vingi anafahamika kwa vibao vyake vingine
vya kuvutia na vilivyoongoza chati, vikiwemo, 'Katchua' na 'K.O', ‘chokolat’, ‘lifobo’
miongoni mwa ngoma nyingine.
Mwaka jana, Ya Levis alijisogeza karibu zaidi na mashabiki
wake wa Kenya alipokuwa mmoja wa watumbuizaji wakuu kwenye tamasha la Raha Fest
lililofanyika mwezi Machi katika uwanja wa Uhuru Gardens.