WAZIRI wa mazingira katika kaunti ya Nairobi, Geoffrey Mosiria ameibua tahadhari kwa wapenzi wa mutura ya kuuzwa mitaani baada ya kudai kumfumania jamaa akiwa na mzoga wa paka.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mosiria alichapisha video
akichakura begi ambalo alisema ni la jamaa ambaye walimkamata.
Mosiria alisema kwamba walimshika jamaa huyo akiwa na begi
safi na baada ya kumsimamisha na kulichakura, walipigwa na butwaa kuona paka
aliyekufa ndani.
Waziri huyo alisema kwamba baada ya uchunguzi wa kina,
walibaini kwamba huenda akawa mmoja wa wachuuzi wa mutura mitaani.
“Wakati wa usimamizi wa
usafi usiku, nilitahadharishwa kuhusu mtu aliyekuwa amebeba paka aliyekufa, na
mara moja, umati wa watu ambao walikuwa wamekusanyika walishuku kuwa anaweza
kuwa mmoja wa wachuuzi wa mtura wanaodaiwa kutumia nyama ya paka kuandaa kitoweo
hicho, wasiwasi uliochochewa na uvumi wa muda mrefu juu ya wauzaji wa vyakula
wasio waaminifu kujihusisha na vitendo hivyo,” alisema.
Mosiria alitoa tahadhari kwa umma kuwa makini na vitoweo vya
mutura wanavyokula na wachuuzi wanaowauzia, akisema kwamba baadhi wanatumia
nyama isiyo halali.
“Ninawasihi kila mtu kuwa waangalifu zaidi kuhusu mahali anaponunua chakula cha mitaani. Ukiona chochote cha kutiliwa shaka, ripoti kwa mamlaka ili kusaidia kudumisha usalama wa chakula na kulinda afya ya umma,” aliongeza.
Waziri huyo amekuwa katika mstari wa mbele kusafisha jiji la
Nairobi usiku na mchana huku akigongana vibega na wamiliki wa vilabu vya starehe,
kanisa na wachafuzi wa mazingira.