MWANAHARAKATI wa haki za kibinadamu nchini Uganda, Winnie Byanyima amemsherehekea mumewe Kizza Besigye katika siku maalum ya kuzaliwa kwake.
Kupitia ukurasa wake wa X, Byanyima
ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la UNAIDS Alifichua kwamba licha ya
mumewe kuzuiliwa gerezani tangu Novemba mwaka jana na kunyimwa haki ya dhamana,
hilo halizuii familia yake kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Byanyima Alifichua kwamba Besigye
ametimiza umri wa miaka 69 na kuweka wazi kwamba amekuwa mhibu wake kwa miaka
32 iliyopita.
“Heri ya kuzaliwa @kizzabesigye, rafiki
yangu mpendwa na mshirika kwa miaka 32 iliyopita! Una miaka 69 leo. Umeishi
maisha ya ujasiri, usadikisho, na kujidhabihu kama nini! Kupigania haki, uhuru,
na utu kwa Waganda wote. Ninajivunia kutembea na wewe. Hapa ni kupenda, kusudi,
na njia ngumu mbeleni. Tutashinda!” Byanyima alimsherehekea.
Besigye amesalia kizuizini tangu
Novemba mwaka jana alipokamatwa kinyemela jijini Nairobi na kusafirishwa hadi
Uganda alikozuiliwa katika gereza la kijeshi.
Hata hivyo baada ya pingamizi kadhaa,
kesi yake ilihamishiwa katika mahakama ya kiraia mnamo Februari na kusomewa
mashtaka ya uhaini ambayo adhabu yake ni kifo.
Hata hivyo, baada ya kukanusha,
aliwekwa katika kizuizi cha gereza moja ambapo amekuwa akisota hadi sasa, baada
ya wiki moja iliyopita kunyimwa dhamana tena.
Wafuasi wake ambao walisubiri kwa hamu
uamuzi ambao ungemsaidia kiongozi huyo mkongwe kuachiliwa kwa dhamana waliachwa
wakiwa wamekata tamaa baada ya Jaji anayesimamia kesi hiyo Rosette Comfort
Kania kuamua vinginevyo.
Mara baada ya hakimu kumaliza kusoma
uamuzi huo, wafuasi hao waliokuwa wamejaza chumba cha mahakama walianza kuimba
kwa sauti kubwa, huku Besigye na washtakiwa wenzake wakijiunga kabla ya
kusindikizwa kurudishwa gerezani.
"Tutashinda, tutashinda, naamini
tutashinda siku moja," wafuasi hao waliimba kwa pamoja, huku wakiinua
mikono juu kuungana na kiongozi wa upinzani.