Afueni ya haraka! Kajala na Marioo waugua siku chache baada ya kuburudika pamoja

Kajala kwa upande wake alidokeza kwamba amepatikana na virusi vya Corona.

Muhtasari

•Siku ya Jumanne, mwanamitindo Paula Kajala aliwatakia wawili hao wa karibu naye afueni ya haraka wanapoendelea kupona.

•Wiki jana, Kajala na Marioo walionekana wakiburudika pamoja kwenye hafla maalum ya usiku wa Paula na Kajala.

katika hafla ya usiku wa Paula na Kajala
Kajala, Marioo na Paula katika hafla ya usiku wa Paula na Kajala
Image: HISANI

Mastaa wawili wa Bongo, muigizaji Fridah Kajala Masanja na mwanamuziki Omary Mwanga almaarufu Marioo wanaugua.

Siku ya Jumanne, mwanamitindo Paula Kajala aliwatakia wawili hao wa karibu naye afueni ya haraka wanapoendelea kupona.

"Get well mama Pau," Paula alimwandikia mama yake kupitia ukurasa wake wa Instagram na kuambatanisha na picha yake.

Mwanamitindo huyo aliambatanisha ujumbe huo na ujumbe mwingine kwa mpenzi wake Marioo akimtakia afueni ya haraka pia.

"Get well my drug (Pona dawa yangu)," aliandika.

Siku ya Jumatatu, taarifa kwenye ukurasa wa Instagram wa Marioo ilifichua kwamba alikuwa mgonjwa na mashabiki wakaombwa kumuombea.

"Tumuombee Marioo," taarifa ilisomeka.

Mamia ya wanamitandao wakiwemo watu maarufu na mashabiki wake walimiminika kwenye chapisho hilo na kumtakia afueni ya haraka.

bensoulmusic Get well soon bro.

chino_kidd Pole sana boss wangu soon utakuwa poa.

shafficomedian Get well soon bro

Baadhi ya wanamtandao wengine hawakuona haya kumuandikia maoni hasi huku baadhi yao wakihusisha maradhi yake na magonjwa ya zinaa.

Kajala kwa upande wake alidokeza kwamba amepatikana na virusi vya Corona.

Kwenye Instastori zake aliandika 'Corona' na kuambatanisha na emoji zinazoashiria huzuni. Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi.

Wiki jana, mastaa hao wawili wa Bongo walionekana wakiburudika pamoja kwenye hafla maalum ya usiku wa Paula na Kajala.

Siku ya Jumatano, muigizajiKajala Masanja na binti yake Paula  waliandaa hafla ya Usiku wa Paula na Kajala ambapo walizindua rasmi Reality Show yao mpya itakayopeperushwa kwenye Zamaradi TV.

Paula aliandamana na mpenzi wake Marioo kwenye hafla hiyo. Wakati hafla ikiendelea, wawili hao walionekana wakipiga gumzo, wakicheza na kukumbatiana kimahaba.

Kwa wakati fulani, alionekana akimpeleka mwanamuziki huyo kwa mama yake Kajala ambaye alimsalimia kwa heshima kabla ya wawili hao kushiriki mazungumzo. Marioo pia aliwatumbuiza wageni kwenye hafla hiyo ambapo muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alijumuika naye kwenye jukwaa ili kucheza pamoja.

"Binadamu ninaowapenda zaidi @kajalafrida @marioo_tz," Paula alisema kuhusu video ya Marioo akicheza na mama yake.

Kajala alionekana mchangamfu na mwenye bashasha tele wakati akicheza na anayedaiwa kuwa mkwe wake jukwaani.

Muigizaji huyo ameonekana kumkubali Marioo kama mkwe wake huku hata akionekana kuwa na muda mzuri naye mara kadhaa ambapo wameonekana wakifanya challenge za ngoma za mwanamuziki huyo.