Akothee aagizwa na mumewe kuacha kazi na kuondoka mitandaoni, kuangazia kupata mimba

Mwimbaji huyo alidokeza kuwa anataka kupata ujauzito kati ya sasa na Julai mwaka huu.

Muhtasari

•Akothee alidokeza madhumuni ya mapumziko yake ya muda usiobainishwa ni kuangazia kuongeza mtoto mwingine.

•Mwimbaji huyo alisifia harusi yake ya mwezi jana huku akibainisha hadhani atawahi kuwa na nyingine nzuri kama hiyo.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee ametangaza mpango wa kuchukua mapumziko kutoka kwa mitandao ya kijamii.

Katika taarifa yake ya siku ya Jumatatu, mama huyo wa watoto watano alidokeza kwamba madhumuni ya mapumziko yake ya muda usiobainishwa yatakuwa kuangazia kuongeza mtoto mwingine.

Aliwaomba mashabiki wake wamruhusu achukue mapumziko akisema anataka kupata mtoto wake wa sita hivi karibuni.

"Sasa nyie mnipe muda. Nitapumzika kutoka kwa kila mtu na kila kitu pamoja na mitandao ya kijamii. Mniruhusu nitafute mtoto wangu wa pili kutoka mwisho, kabla hatujazungumza mambo mengine.  Nataka kuwa mama mwaka huu," Akothee alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alisema mume wake Denis Shweizer almaarufu Omosh amemwagiza aache kazi, aondoke kwenye mitandao ya kijamii na aondoke Kenya kabla ya siku ya Ijumaa.

Alidokeza kuwa anataka kupata ujauzito kati ya sasa na Julai mwaka huu kwani daktari wake tayari alikuwa amemueleza ingekuwa vigumu kupata mimba mara tu baada ya harusi yake iliyofanyika Aprili 10.

"Hatujapata wakati wa kwenda kwa honey Moon. Siku zinakwenda na mwaka unakaribia kuisha. Hatuna mimba bado, nadhani nina stress sana. Kwa hivyo ninataka kushikilia kila kitu na kuzingatia maisha yangu ya mapenzi.

Nisiposhika mimba kati ya sasa na Julai, kila mengine yatasubiri, Dr @swaleh__md aliniambia nishikilie mpaka baada ya harusi, aliniambia wazi kuwa harusi humaliza nguvu kwahiyo naweza nisipate mimba hivi karibuni au naweza kupoteza ujauzito tena. Nilipopata hedhi nilijikasirikia. Daktari ulikuwa sahihi," alisema.

Mwimbaji huyo alisifia harusi yake ya mwezi jana huku akibainisha hadhani atawahi kuwa na nyingine nzuri kama hiyo.

Alibainisha kuwa yeye na mumewe wamekuwa na shughuli nyingi baada ya harusi hivi kwamba hawajapata wakati wa kufungua zawadi.

"Mume wangu aliondoka kwenda kazini mara baada ya mapumziko ya wiki mbili," alisema.

Mwimbaji Akothee na mchumba wake Dennis Shweizer almaarufu Mister Omosh walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, Nairobi mnamo Aprili 10, 2023. Harusi hiyo yake ya pili ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii na wanasiasa mashuhuri nchini. Jumla ya watu wasiopungua 300 walialikwa kwenye hafla hiyo ya kufana.