Amira adokeza mahusiano na bwenyenye mwingine baada ya kumtema Jimal Rohosafi

Mama huyo wa watoto wawili alishiriki video ya mwanamume huyo akimchukua kwa Range Rover Vogue 2023.

Muhtasari

•Bi Amira pia anaonekana kusonga mbele na maisha yake sasa kulingana na chapisho lake la hivi punde.

•Amira alichapisha video ya mwanamume ambaye alidai alikuja kumchukua kwenye gari aina ya Range Rover.

Jimal Rohosafi na aliyekuwa mke wake Amira
Image: HISANI

Huenda mfanyibiashara Amira amezama tena kwenye dimbwi la mahaba zaidi ya mwaka mmoja baada ya kugura ndoa yake na Jimal ‘Marlow’ Rohosafi.

Ndoa ya wawili hao ya miaka mingi ilisambaratika mwishoni mwa mwaka 2021 baada ya Jimal kuonekana kumpendelea zaidi na kumchagua aliyekuwa mke wake wa pili, mwanasoshalaiti Amber Ray, badala ya mzazi huyo mwenzake.

Baada ya kutengana na Amira, mwanzilishi huyo wa Huduma Credit aliendelea kuchumbiana na Amber Ray kwa muda kabla ya wawili hao kutengana baadaye kwa njia ya kutatanisha. Baadaye alijitosa kwenye mahusiano na rafiki yake wa karibu Michelle Wangari ambaye alizaa naye mtoto mapema mwaka huu.

Naam, mapya ni kuwa Bi Amira pia anaonekana kusonga mbele na maisha yake sasa kulingana na chapisho lake la hivi punde.

Siku ya Alhamisi, akiwa Dubai kwa ajili ya kufanya manunuzi, alichapisha video ya mwanamume ambaye alidai alikuja kumchukua kwenye gari aina ya Range Rover. Hata hivyo hakutoa maelezo wala sura ya mwanamume huyo.

"Anapokuja kukuchukua kwenye gari la Range Rover Vogue 2023 autobiography," Amira alisema kwenye video aliyochapisha.

Aliongeza, "Niskie mtu akisema amevaa socks na open shoes."

Mama wa watoto wawili wavulana alionyesha tu miguu ya mwanaume huyo asiyejulikana na ambaye anaonekana kuwa tajiri.

Image: INSTAGRAM// BEING AMIRA

Haya yanajiri takriban mwaka mmoja unusu baada ya mfanyibiashara huyo wa vipondozi kugura ndoa yake na Jimal Rohosafi.

Mapema mwaka huu, wazazi wenza hao walihusika katika vita vya maneno hadharani baada ya Amira kusema anajuta kupata watoto na mwanzilishi huyo wa Huduma Credit kwa madai kuwa ni mwanamume mkatili. 

 Katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, mama huyo wa wavulana wawili alidai kuwa Jimal aliwahi kumpiga wakati akiwa mjamzito, madai ambayo Jimal alikanusha.

Julai mwaka jana, Jimal alimuomba radhi mama huyo wa watoto wake wawili kwa drama nyingi alizosababisha kwenye ndoa yao mwaka 2021.

Katika ombi lake, Jimal alikiri kuwa alimkosea sana mkewe kwa kutekeleza wajibu wake wa kumlinda. Alimuomba Amira apokee ombi lake la msamaha huku akimkumbusha jinsi ambavyo wamepitia mengi pamoja.

"Ilikuwa mbaya kabisa. Huenda nilionekana kama mtu asiye na wasiwasi lakini sikuwa na la kufanya. Nilijua haikuwa sawa, nilijua unaumia lakini sikuweza kujikusanya!Amira nafanya hivi kwa sababu ukosefu wa heshima pia ulikuwa mkubwa. Naomba radhi kwa kukosa heshima," Aliandika.

Katika jibu lake, Amira alisema hawezi kuuelewa msamaha wa mzazi mwenzake kwani ulifufua kumbukumbu ya siku mbaya za nyuma.

"Ombi hilo la msamaha limenirudisha katika sehemu moja ya giza ambayo nimewahi kuwa katika maisha yangu kwa sababu nimetafakari juu ya mengi yaliyotokea hadharani na nyuma ya milango iliyofungwa na imezua hisia nyingi," alijibu.

Mfanyibiashara huyo aliomba neema ya Mungu huku akitafakari suala hilo na kueleza kuwa kwa sasa amezidiwa na hisia.