Staa wa Mugithi Samuel Muchoki Ndirangu almaarufu Samidoh alijibu kwa kejeli baada ya mtumiaji wa Facebook kumshutumu kwa kuharibu maisha ya aliyekuwa mke wake, Edday Nderitu.
Baba huyo wa watoto watano mnamo Jumapili asubuhi alishiriki chapisho la ucheshi kuwaburudisha mashabiki wake wa mtandaoni na akashirikisha baadhi yao kwenye sehemu ya maoni.
"Jamani, 'mpenzi mkali ni kwa matajiri, mimi niliambiwa ni mpenzi sumu na sijiamini. Aki Kanairo wewe,” Samidoh aliandika kwenye picha yake akiwa na wanasiasa kadhaa.
Chini ya chapisho hilo, shabiki mmoja alichukua fursa hiyo kumshutumu kwa kuharibu maisha ya mama wa watoto wake watatu.
"Umeharibu maisha ya Edday," mtumiaji wa mtandao wa Facebook, Robert Ke, aliandika.
Katika majibu yake, mwimbaji huyo wa Mugithi alidokeza kwamba mke huyo wake wa zamani ambaye amekuwa akiishi Marekani katika miezi kadhaa iliyopita anaendelea vyema zaidi.
"Robert Ke, anaendelea vizuri kuliko baba yako," Samidoh alisema.
Wanamtandao wengi waliofikiwa na ujumbe huo walionekana kushtushwa na kufurahishwa na majibu ya mwimbaji huyo.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya mwimbaji huyo wa Mugithi kufunga safari hadi Marekani kuwatembelea watoto wake watatu na aliyekuwa mkewe, Edday Nderitu. Wanandoa hao wawili wa zamani wanaaminika kukutana na kuzungumza wakati wa ziara hiyo fupi ya mwezi uliopita.
Mke wa msanii huyo wa miaka mingi, Edday Nderitu kwa sasa anaishi Marekani pamoja na watoto wao. Aliondoka nchini mapema mwaka jana na anaonekana tayari kutulia huko vizuri huku watoto wakiwa wameanza shule huko.
Mwezi Julai mwaka jana, Bi Edday Nderitu aliweka wazi kwamba alimuacha mumewe ili awe na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.
"Wacha nifafanue mambo machache ambayo yalishirikiwa mtandaoni na sio sahihi. Siko kwenye ndoa ya wake wengi, kama ilivyoelezwa nilimuacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi,” Edday alisema kupitia Facebook.
Aliongeza, "Nilifanya uamuzi wa kujiondoa mimi na watoto wangu kutoka kwa mazingira hayo yenye sumu, haswa binti yangu kijana ambaye kwa bahati mbaya anapokea moja kwa moja tabia isiyoaminika iliyoonyeshwa."
Mara nyingi, Bi Edday Nderitu amesisitiza kwamba hayuko tayari kuwa kwenye ndoa ya wake wangi licha ya mpenzi wa Samidoh, seneta Karen Nyamu kusisitiza kwamba yuko tayari ku'share mume naye.