"Bado nalia!" Njoro, Jalang'o, Awinja wamkumbuka kwa hisia marehemu Papa Shirandula

Bukeko alifariki mnamo Julai 18, 2020 akiwa na umri wa miaka 58 na kuacha pengo kubwa sana katika tasnia ya filamu.

Muhtasari

•Jalang’o alisimulia jinsi alivyopata habari kuhusu kifo cha Papa Shirandula na kufichua kwamba yeye na waigizaji wenzake hawakupata fursa ya kumuaga.

•Njoro ambaye aliigiza kama rafiki mkubwa wa marehemu alifichua kuwa bado anaomboleza kifo chake miaka mitatu baada ya kumzika.

Marehemu Charles Bukeko almaarufu Papa Shirandula
Image: HISANI

Miaka mitatu iliyopita, muigizaji mashuhuri Charles Bukeko almaarufu Papa Shirandula alizikwa baada ya kufariki kutokana na ugonjwa wa Covid 19.

Bukeko alifariki mnamo Julai 18, 2020 akiwa na umri wa miaka 58 na kuacha pengo kubwa sana katika tasnia ya filamu nchini Kenya. Alizikwa nyumbani kwake katika kijiji cha Namisi-Bukeko eneo la Funyula kaunti ya Busia katika hafla ya maziko iliyohudhuriwa na wanafamilia wa karibu na marafiki wachache wakiwemo waigizaji wenzake.

Waliokuwa waigizaji wenzake katika kipindi cha Papa Shirandula kwenye runinga ya Citizen TV Phelix Odiwour (Jalang’o), Jacky Vike (Awinja) na Kenneth Gichoya (Njoro) wametumia siku hii, Julai 20 kumkumbuka na kutambua jukumu kubwa alilocheza maishani mwao.

Jalang’o alisimulia jinsi alivyopata habari kuhusu kifo cha Papa Shirandula na kufichua kwamba yeye na waigizaji wenzake hawakupata fursa ya kumuaga kwani kila kitu kilifanyika haraka sana.

Pia ameshiriki kipande cha video ya kumbukumbu  ambapo anaonekana akifanya mazungumzo na marehemu katika moja ya vipindi vya sinema hiyo maarufu ya vichekesho na kuitakia roho yake amani akiendelea kupumzika.

“Pumzika kwa amani Baba! Asante kwa kila jambo,” Jalang’o aliandika.

Kwa upande wake, Njoro ambaye aliigiza kama rafiki mkubwa wa marehemu alifichua kuwa bado anaomboleza kifo chake miaka mitatu baada ya kumzika.

"Miaka mitatu iliyopita siku kama ya leo tulimzika Papa Shirandula. Bado ninalia kaka yangu mkubwa. Endeleeni kupumzika kwa amani,” Njoro alisema.

Awinja alimtaja mchekeshaji huyo marehemu kama baba yake na akafichua kuwa kumpoteza ilikuwa mojawapo ya nyakati mbaya zaidi katika maisha yake.

Aliendelea kuzungumzia jukumu kubwa la Papa Shirandula katika maisha yake na ya wengine wengi na akamthamini marehemu kwa kila kitu.

 “Miaka mitatu iliyopita leo tulimzika baba yetu Papa Shirandula, ikiwa bado ni moja ya siku ya giza sana maishani mwangu, lakini namsherehekea hata hayupo. Alitugundua wengi wetu, nashukuru,” alisema.

Awinja aliongeza, "Endelea kupumzika Papsy, Mzae urithi wako unaendelea!"

Roho ya Papa Shirandula iendelee kupumzika kwa amani. Alituburudisha na kupasua mbavu zetu kwa miaka mingi.