Betty Kyallo alazimika kutoa pesa nyingi baada ya kutishiwa kuanikwa na mtu aliyekuwa amemkopesha

Mwanahabari huyo alisema kwamba kuwa na deni ni jambo la kawaida kwa mtu yeyote akiwemo yeye.

Muhtasari

•Betty amesimulia alivyolazimika kutoa kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa akaunti yake baada ya rafikiye mmoja kutishia kumtangaza hadharani kuwa na deni lake.

•Betty alibainisha kuwa pia kuna watu wenye deni lake, baadhi yao ambao hawajamlipa bado muda mrefu baada ya kukopa.

Image: INSTAGRAM// BETTY KYALLO

Aliyekuwa mtangazaji wa habari za TV, Betty Kyallo amefichua kwamba yeye pia hukumbwa na matatizo ya kawaida kama mtu mwingine yeyote.

Wakati akizungumza kwenye chaneli yake ya mtandao wa YouTube ambapo alikuwa akijibu baadhi ya maswali ya mashabiki wake, Betty alifunguka kuhusu tatizo la kifedha ambalo alikumbana nalo hivi majuzi.

Mama huyo wa binti mmoja alisimulia alivyolazimika kutoa kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa akaunti yake ya benki baada ya rafiki yake mmoja aliyekuwa amemkopesha pesa kutishia kumtangaza hadharani kuwa na deni lake.

“Mtu huyo alinipigia simu na kuniambia bora nimlipe deni lake la sivyo atanitangaza wazi kwenye mitandao ya kijamii. Nilijiambia, ni kazi nyingi kwenda kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu sijali mambo hayo. Lakini nikajiambia, mwisho wa siku, sikuwa nitoroke, ningelipa kwa sababu tuko kwenye mawasiliano, sisi ni marafiki. Siku moja tu unaamka unasema nataka yote leo. Hilo halifai,” Betty Kyallo alisimulia.

Aliendelea, "Ilinibidi niende kwenye akaunti yangu na kutoa kiasi kikubwa cha pesa, sitasema ni kiasi gani. Ilinibidi kuwalipa kwa kweli ili wasije kunichafulia jina langu. Sio kama nilikuwa na pesa hizo, sio eti pesa nilizolipa hazikungoja kufanya chochote. Hiyo ndiyo pesa iliyopangiwa. Lakini unakabiliana vipi na maisha? Imenishika hivyo leo, nimepatwa, unang’ang’ana nayo. Ama unaongelesha huyo mtu atulie ama unawalipa.

Mfanyibiashara huyo ambaye anaendesha Flair by Betty alisema kwamba kuwa na deni ni jambo la kawaida kwa mtu yeyote akiwemo yeye.

Kwa upande mwingine, alibainisha kuwa pia kuna watu wenye deni lake, baadhi yao ambao hawajamlipa bado muda mrefu baada ya kukopa.

"Ni kawaida sana kudaiwa pesa na watu, ndivyo tunavyoishi katika nchi hii. Hata kuna watu nawadai pesa nyingi sana, nina watu ambao bado ninawafukuza karibu kama miaka 2/3 baadaye. Ni sawa kuwa na deni, ni kawaida kuwa na deni. Hata Kenya ina deni,” alisema.

Aidha, Betty amewashauri watu kujifunza jinsi ya kukabiliana na masuala ya kimaisha jinsi yanavyokuja, kuchukua hatua moja baada ya nyingine na kuepuka kukumbatia vitu vingi kwenye sahani zao.