Bintiye Diamond, Latifah Dangote ambwagia sifa kemkem mama yake Zari Hassan

Tiffah amemsherehekea Zari kwa kuwa kuwa mama bora kwake.

Muhtasari

•Latifah aliandika ukurasa mzima wa kitabu kumsifu mwanasoshalaiti huyo kutoka Uganda kwa kuwa mama bora kwake.

•Punde baada ya kusoma ujumbe huo Zari alimpiga bintiye busu kwenye shavu lake kutokana na furaha iliyomjaa moyoni.

Image: INSTAGRAM// PRINCESS TIFFAH

Asubuhi ya Jumapili Latifah Dangote  alimuamsha mama yake Zari Hassan mapema sana ili kumtakia kheri za siku ya kina mama.

Katika video ambayo Zari alipakia Instagram, Tiffah ambaye ni binti wa mwanasoshalaiti huyo na staa wa Bongo Diamond alionekana akiwa amebeba kitabu alichokuwa amemwandikia mamake jumbe tamu.

"Habari za asubuhi. Mbona waniamsha mapema hivi ukikaa vizuri? Oh, kumbe ni siku ya kuadhimisha kina mama. Aaw Latifah, Shukran inakaa vizuri," Zari alisikika akisema punde baada ya kuamshwa na bintiye.

Kwa kawaida, kila mwaka ifikapo Mei 8 dunia huadhimisha siku ya kina kina mama. Walimwengu hutumia mbinu tofauti kuwasherehekea kina mama zao.

Latifah aliandika ukurasa mzima wa kitabu kumsifu mwanasoshalaiti huyo kutoka Uganda kwa kuwa mama bora kwake.

"Mama yangu ana kipaji. Yeye ni mchangamfu sana, anayejali, mwenye furaha, mwerevu, mwenye busara, mtamu, mkarimu, anafurahisha, mtulivu, mzuri, mkuu, mwenye upendo na ni shujaa wangu," Latifah alimwandikia mamake.

Punde baada ya kusoma ujumbe huo Zari alimpiga bintiye busu kwenye shavu lake kutokana na furaha iliyomjaa moyoni.

Latifah ni binti wa Zari na Diamond Platnumz kutoka kwa ndoa yao iliyodumu kwa takriban miaka minne.

Alizaliwa mnamo Novemba 6, 2015 na kuwa mtoto wa nne wa Zari ambaye kwa sasa ana watoto watano kwa jumla.

Ingawa mahusiano yao yalifika kikomo, Zari na Diamond wameendelea kushirikia vizuri katika malezi ya Tiffah na ndugu yake Prince Nillan.