Daddy Owen aonywa vikali kuhusu kibarua kigumu cha kuchumbiana na Charlene Ruto

Butita alimwambia Owen itakuwa rahisi kwake kunaswa ikiwa ata'cheat kwani bintiye rais atatumia mamlaka za serikali kumchunguza.

Muhtasari

•Butita amemuonya mwimbaji Daddy Owen ambaye anadaiwa kuchumbiana na binti ya Rais Willam Ruto, Charlene Ruto.

•Butita alidai kuwa wanajeshi watatumiwa kutatua maswala ya ndoa kwani wazazi wa Charlene watakuwa na shughuli nyingi kutumikia taifa.

amemuonya Daddy Owen kuhusu matatizo ya kuchumbiana na Charlene Ruto
Butita amemuonya Daddy Owen kuhusu matatizo ya kuchumbiana na Charlene Ruto
Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji maarufu wa Kenya Eddie Butita amemuonya mwimbaji wa nyimbo za injili Owen Mwatia almaarufu Daddy Owen ambaye anadaiwa kuchumbiana na binti ya Rais Willam Ruto, Charlene Ruto.

Katika video ambayo alishiriki kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Butita alibainisha kuwa kumekuwa na tetesi nyingi zikimuhusisha mwanamuziki huyo mahiri kimapenzi na Bi Charlene.

Mchekeshaji huyo alisema iwapo tetesi hizo ni za kweli, basi Daddy Owen yuko kwenye shida kubwa kwani uhusiano huo utakuwa wa kazi ngumu zaidi.

“Daddy Owen wewe ni rafiki yangu, wacha nikwambie. Kuchumbiana na binti ya rais, kama unachumbiana na Charlene. Hiyo sio kuchumbiana, hiyo ni kazi. Hiyo ni wajibu, kama kulipa ushuru,” alisema Butita.

Aliendelea kumweleza kuwa itakuwa rahisi sana kwake kunaswa ikiwa ataenda nje ya mahusiano kwani kulingana naye, bintiye rais atatumia mamlaka za serikali kumchunguza.

“Huyo hata hajahitaji nywila kuona jumbe zako. Hawa kwa wako na DCI, wako na NIS. Yaani wewe ni simu tutapata unapata kutoka Barabara ya Kiambu, unaambiwa “Hallo, hapa ni DCI. Huyu Carol ni nani?" Yaani wewe jua saa hii ni mapenzi ambayo ni kazi,” alisema.

Aliongeza, “ Hakuna kufuriana kwa nyumba. Mnafura kidogo alafu uone Subaru inakufuata. Nakuambia utalia kwa hiyo barabara eti “Mbona, mbona, mbona”

Mchekeshaji huyo pia alidai kuwa wanajeshi watatumiwa kutatua maswala ya ndoa kwani wazazi wa Charlene watakuwa na shughuli nyingi kutumikia taifa.

“Hapo hakuna ati kusuluhisha matatizo ya ndoa na wazazi. Mzazi ako bize, mzazi ni rais. Mkiwa na shida ni D.O.D. Chini ya ulinzi mkubwa. Uende uambie mamlaka mkuu wa jeshi kwa nini unakasirisha mtoto wa amri jeshi mkuu. Eti nipee dakika tatu niambie hawa majeshi.. Hiyo saluti yako ulikuwa unapiga muziki. Buda unaenda kuona moto,” Butita alimwambia Daddy Owen.

Alimalizia kwa kumwambia mwanamuziki huyo, “Lakini kila la kheri kama ni ukweli. Na kama ni uwongo fanya bidii iwe ni ukweli.”

Katika miezi michache iliyopita, kumekuwa na madai mengi kwamba Daddy Owen na Charlene Ruto wanachumbiana baada ya wawili hao kuonekana wakiandamana sana.

Hapo awali, Daddy Owen alikuwa amekanusha uhusiano wowote wa kimapenzi na Charlene lakini mwezi uliopita iliripotiwa kwamba mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alimpeleka binti huyo wa rais kwa wazazi wake na kumtambulisha kwao.