"Tunalala na viatu!" Raila Odinga na Paul Kagame washerehekea ushindi wa Arsenal dhidi ya Tottenham kwa bashasha tele

Muhtasari

•Raila alipakia video ambayo ilikuwa imerekodiwa mapema siku ya Jumapili kabla ya mechi kuchezwa ambapo alikejeli  mashabiki wa United kwa kupata kichapo cha 0-1 dhidi ya Aston Villa siku ya Jumamosi.

•Kwa upande wake Kagame alipongeza meneja Mikel Arteta, wachezaji na mashabiki kufuatia ushindi huo.

Image: HISANI

Jumapili ya Septemba 27 itabaki kuwa siku ya kukumbukwa  na mashabiki wa klabu ya Arsenal.

Wanabunduki waliweza kupata ushindi mkubwa wa 3-1 dhidi ya mahasidi wao wa jadi Tottenham Hotspurs, jambo ambalo limeridhisha mashabaki kote dunia nzima.

Miongoni mwa mashabiki  sugu wa klabu hiyo ya London ambao  walieleza furaha yao kufuatia ushindi huo ni pamoja na aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga na rais wa Rwanda Paul Kagame.

Punde baada ya mechi hiyo ambayo ilichezewa ugani Emirates kutamatika, kinara wa ODM alipakia picha mitandaoni iliyoonyesha akisherehekea ushindi huo mbele ya runinga.

"Tumerudi kwa nyakati za ushindi! Vizuri sana @Arsenal" ndio ujumbe ambao Raila aliambatanisha picha hiyo nao.

Image: TWITTER// RAILA ODINGA

Dakika chache baadae alipakia video ambayo ilikuwa imerekodiwa mapema siku ya Jumapili kabla ya mechi kuchezwa ambapo alikejeli  mashabiki wa United kwa kupata kichapo cha 0-1 dhidi ya Aston Villa siku ya Jumamosi.

"Yule alinialika Man U, namwambia jana mliona Aston Villa. Walisalimu nyinyi sana. Mimi ni Arsenali, leo tutapigana na Tottenham" Raila alisema kwenye video hiyo.

Kwa upande wake Kagame alipongeza meneja Mikel Arteta, wachezaji na mashabiki kufuatia ushindi huo.

Rais huyo wa nchi jirani alitakia klabu hiyo ya moyo wake ushindi katika mechi zijazo.

"Pongezi mahali ifaapo. Hongera Arsenal, meneja, wachezaji na mashabiki!! Kila kitu kilikuwa hai leo. Heri njema kwa mechi zote" Kagame aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Wawili hao wamekuwa wakishabikia Arsenal kwa miaka mingi licha ya misururu ya matokeo duni kwenye misimu ya hivi karibuni ya EPL.