"Sisi ni marafiki" Nadia Mukami afichua siri inayofanikisha zaidi mahusiano yake na Arrow Bwoy

Muhtasari

•Malkia huyo wa muziki wa kisasa amesema kwamba wakati anapokuwa na mpenzi wake yeye huwa msichana tu wa kawaida ambaye anatekeleza majukumu yake kwenye uhusiano kikamilifu.

•Kulingana na Nadia, suala la muhimu zaidi  kwenye uhusiano sio wapenzi kushinda wameambiana jinsi wanavyopendana ila ni kusaidiana  na kushauriana wakati tatizo lolote linapotokea.

Image: INSTAGRAM//NADIA MUKAMI

Mwanamuziki Nadia Mukami amefichua kuwa sababu kubwa ya mahusiano yake na Arrow Bwoy kufanikiwa ni kwa sababu wao ni marafiki.

Akiwa kwenye mahojiano na Gerry Wainaina kwenye ukurasa wa Mkenya Marekani katika mtandao wa YouTube, Nadia alisema kuwa umaarufu wake huisha punde anapofika mlangoni wa nyumba yake.

Malkia huyo wa muziki wa kisasa amesema kwamba wakati anapokuwa na mpenzi wake yeye huwa msichana tu wa kawaida ambaye anatekeleza majukumu yake kwenye uhusiano kikamilifu.

"Umaarufu huwa wakati ninapotumbuiza jukwaani tu. Wakati tuko na yeye mimi huwa msichana wa kawaida tu.  Mwisho wa siku nataka familia, nataka nipike, nataka niulizwe mbona sijaosha vyombo na niombe msamaha. Nataka familia. Sijasema eti upige magoti, pia mimi ni kichwa ngumu kwa wakati mwingine lakini lazima ninyenyekee kidogo ninapofika kwa nyumba" Nadai alisema.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 24 amesema kuwa  kuna urafiki mkubwa kati yake na mpenziwe.

Kulingana na Nadia, suala la muhimu zaidi  kwenye uhusiano sio wapenzi kushinda wameambiana jinsi wanavyopendana ila ni kusaidiana  na kushauriana wakati tatizo lolote linapotokea.

"Sababu kuu uhusiano wangu na Arrow umefanikiwa ni kwa kuwa sisi ni marafiki. Suala la kushinda mmeambiana eti nakupenda mara kumi kwa siku sio lazima.Unafaa ujiulize ikiwa nyinyi ni marafiki ambao wanaweza  kushauriana wakati mmoja wenu anapokabiliwa na tatizo. Anaweza kuwa amenikosea nimwambia amenichosha. Uzuri ni kuwa yeye ni rafiki" Alisema Nadia.

Kama dhihirisho la mapenzi yake kwa Arrow Bwoy, Nadia alisema kuwa ata'propose' mwenyewe iwapo  mpenzi  wake atakosa kuchukua hatua hiyo.