Hisia ya ladha ya King Kaka haijarejea bado baada ya kuwa anaugua kipindi kirefu- mkewe Nana Owiti afichua

Muhtasari

•Hata hivyo mwanamuziki huyo ameendelea kupata afueni haswa katika kipindi cha mwezi mmoja ambacho kimepita.

•Mpenzi wake Nana Owiti amefichua kuwa huwa analazimika kuonja chakula chake kuhakikisha kuwa hakina viungo kabla ya kumpatia akule

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwanamuziki Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka amekuwa akiugua kwa kipindi cha takriban miezi minne ambayo imepita.

Mapema mwezi uliopita rapa huyo alifichua kwamba vipimo vibaya na madawa ambayo alipatiwa na daktari katika hospitali moja nchini yalimsababishia madhara mabaya mwilini.

Kaka alieleza kwamba aliugua maradhi ambayo yalimfanya apoteze kilo 33, apoteze hisia ya ladha, kiuno chake kupungua kati ya dalili zingine.

Hata hivyo mwanamuziki huyo ameendelea kupata afueni haswa katika kipindi cha mwezi mmoja ambacho kimepita.

Tayari ametangaza kuwa ameongeza uzito kiasi mwilini baada ya kupoteza kiwango kikubwa cha uzito ndani ya miezi mitatu aliyokuwa ameathiriwa vibaya na ugonjwa. 

"Haijalishi ushindi ni mdogo kiasi gani bado ni ushindi tu uliangalia uzito wangu na nimepata kilo 6. Kupotezakilo zote hizo haikuwa utani na sasa kuona faida ni motisha kubwa na baraka. Asante kila mtu ambaye alisali Twendelee ubarikiwe. " Mwanamuziki huyo alitangaza kupitia mtandao wa Instagram wiki iliyopita.

Ingawa King Kaka amepiga hatua kiasi katika safari yake ya kupata afueni kikamilifu, ni dhahiri kuwa bado hisia yake ya ladha haijarejea kikamilifu.

Mpenzi wake Nana Owiti amefichua kuwa huwa analazimika kuonja chakula chake kuhakikisha kuwa hakina viungo kabla ya kumpatia akule.

Bi Owiti alisema kuwa hali hiyo imefanya wasite kula hotelini tena ama kutoa maagizo kwa wapishi kuhusu namna chakula cha King Kaka kinafaa kutayarishwa.

"Hisia ya ladha ya @thekingkaka haijarejea kabisa kwa hivyo huwa naonja chakula chake kuhakikisha kuwa hakuna viungo. Ni vigumu sana tule hotelini isipokuwa tu tutoe maagizo kabla kuhusu jinsi chakula kinafaa kutayarishwa  na lazima niwe pale. Vinginevyo tunakula nyumbani kwetu ama kwa mama yake" Bi.. Owiti alifichua kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Nana amesema kuwa mtazamo wao wa maisha ulibadilika kufuatia yale yote ambayo yamejiri  na kudai kuwa sasa wanasherekea hali ya kuwa hai kila siku.

"Kila siku kwetu ni siku ya kusherehekea uhai. Sasa tunatazama maisha vitofauti. Tunahesabu baraka zetu. Tunatengeneza muda kwa wale ambao tunajali. Tunakula pamoja mara kwa mara" Alisema Nana.

Asubuhi ya Jumatano King Kaka alisuta vikali mwanablogu ambaye alikuwa amechapisha habari za uongo eti alikuwa amebakisha muda mfupi duniani.

Picha ambayo alipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram ilionyesha habari zilizodai kuwa alikuwa ameaga Wakenya kwaheri kwa kuwa daktair alikuwa amemuarifu kuwa amebakisha mwezi mmoja wa kuishi.

"Shida ya blogs  huwa nini? Mbona uandike kitu kama hiyo? Hata hivyo ata adui ambaye ako na shida ya kulala halala kweli." Kaka aliandika chini ya ujumbe huo.

Wanamitandao wengi walijumuika kumkashifu mwanablogu aliyekuwa ameandika habari hizo za uongo.