Fahamu kwa nini Boniface Mwangi na mwanawe waliacha kuvaa bangili zenye rangi za bendera ya Kenya

Mwangi alilalamika kwamba rais ana mazoea ya kutumia mamlaka yake vibaya na kukandamiza raia

Muhtasari

•Baba huyo wa watoto watatu alidai kwamba nchi ya Kenya inachosha raia wake sana na kudai kuwa aliachia rais Kenyatta tamaduni ya kuvaa bangili ya Kenya.

•Kwa upande wake Nate Simphiwe alisema kwamba aliacha kuvaa bangili ya Kenya wakati alipogundua kuwa maisha ni magumu sana humu nchini

Image: INSTAGRAM// BONIFACE MWANGI

Mwanaharakati mashuhuri Boniface Mwangi pamoja na mwanawe Nate Simphiwe wamedhihirisha wazi kwamba waliacha kuvaa bangili zenye rangi za bendera ya Kenya kama ilivyo ada ya raia wengi nchini.

Kupitia video ambayo Mwangi alipakia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, wawili hao walidai kwamba walifanya maamuzi hayo kufuatia masaibu chungu nzima yaliyojaa nchini Kenya.

Baba huyo wa watoto watatu alidai kwamba nchi ya Kenya inachosha raia wake sana na kudai kuwa aliachia rais Kenyatta tamaduni ya kuvaa bangili ya Kenya. Mwangi alilalamika kwamba rais ana mazoea ya kutumia mamlaka yake vibaya na kukandamiza raia.

"Hii nchi inanyanyasa raia wake sana kusema kweli. Hii nchi inachosha. Kama mtoto wa miaka kumi na minne alichoshwa na nchi hii na aliacha kuvaa bangili yake, mbona mimi nivae. Niliacha kuvaa bangili ya Kenya, mimi sivai hiyo kitu. Nilichia Uhuru avae pekee yake kwa sababu anatumia nchi hii kama mali yake ya kibinafsi. Uhuru, nchi ni yako chukua. Hata hati ya hatimiliki  ya Kenya tumekupatia chukua" Mwangi alisema.

Kwa upande wake Nate Simphiwe alisema kwamba aliacha kuvaa bangili ya Kenya wakati alipogundua kuwa maisha ni magumu sana humu nchini

Nate ambaye ana umri wa miaka 14 alidai kwamba tangu alipoacha kuvaa bangili hiyo aligundua kwamba ako tayari kuhama nchi kwa wakati wowote ule.

Kitambo nilidhani nchi nilidhani nchi itabadilika kuwa nzuri. Kisha nikawa mkubwa na nikagundua kwamba maisha sio jua na pipi. Ile siku niliacha kuvaa bangili ya Kenya niligundua kwamba niko tayari kuhama nchi hii, ukisema tuende tutaenda" Alisema Nate.

Hivi majuzi mwanaharakati huyo amekuwa akishambuliwa sana mitandaoni haswa kwa kujihusisha sana na uhusiano wa Juliani na aliyekuwa mpenzi wa gavana Mutua, bi Lilian Ng'ang'a.