"Mimi sio shabiki wa ngono!" Eric Omondi aapa kuhifadhi ubikira wake hadi atakapofunga ndoa

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo alieleza kwamba kipaumbele chake kwa sasa ni kazi yake tu huku akidai kuwa mapenzi yanaweza kufanya apoteze mwelekeo.

•Msanii huyo ambaye hivi majuzi alizindua onyesho la tatu la shoo ya Wife Material ametoa ombi kwa watu waheshimu uamuzi wake.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji mashuhuri nchini Eric Omondi amewaacha wengi vinywa wazi baada ya kuapa hadharani  kuwa atajihifadhi hadi wakati atakapofunga ndoa.

Omondi amesema kwamba kitendo cha ndoa sio kitu ambacho amepatia kipaumbele maishani mwake na kudai kuwa yeye sio shabiki wa ngono.

Kwenye video ambayo alipakia katika ukurasa wake wa Instagram, mchekeshaji huyo alieleza kwamba kipaumbele chake kwa sasa ni kazi yake tu huku akidai kuwa mapenzi yanaweza kufanya apoteze mwelekeo.

Amesema kwamba hatazamii kushiriki tendo la ndoa na yeyote kwa sasa hadi atakapopiga hatua ya kufunga pingu za maisha.

"Mimi sio mpenzi. Mimi sio shabiki wa ngono. Ngono sio kitu ambacho huwa  nafikirikia ama ningependa kufanya. Mimi ni mchekeshaji anayezingatia kazi yake, ndio maana wananiita rais wa vichekesho. Kwa sasa sidhani ngono ni kipaumbele changu. Nataka kuzingatia kazi yangu. Nadhani ngono ni kitu cha kufanya nipoteze mwelekeo.  haswa kabla ya ndoa. Nataka kujihifadhi nikiwa bikra" Eric alisema.

Msanii huyo ambaye hivi majuzi alizindua onyesho la tatu la shoo ya Wife Material ametoa ombi kwa watu waheshimu uamuzi wake.

"Nimeamua kuhifadhi ubikra wangu hadi nitakapofunga ndoa na natumai watu wataheshimu uamuzi wangu" Omondi aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Hata hivyo wengi wamepata matamshi ya mchekeshaji huyo kuwa tatanishi kwani tayari amekuwa kwa mahusiano  kadhaa na hata inajulikana wazi kwamba ana mtoto mmoja ambaye alipata pamoja na mtangazaji Jackie Maribe.