"Maisha yangu yalibadilika ulipowasili" Mulamwah aandikia bintiye ujumbe maalum huku akifichua sura yake hadharani kwa mara ya kwanza

Muhtasari

•Mulamwah pamoja mpenzi wake Caroline Muthoni walipakia picha maridadi ya Keilah Oyando  kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii na kuambatanisha na jumbe maalum.

•Mulamwah ameapa kupatia maslahi ya bintiye kipaumbele kila wakati huku akimtakia maisha marefu na  baraka tele maishani.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah hatimaye ametambulisha sura ya bintiye hadharani kwa mara ya kwanza tangu alipozaliwa takriban mwezi mmoja uliopita.

Mulamwah pamoja mpenzi wake Caroline Muthoni walipakia picha maridadi ya Keilah Oyando  kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii na kuambatanisha na jumbe maalum.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 28 alisema kwamba maisha yake yalibadilika punde baada ya binti yake kuzaliwa.

Ameapa kupatia maslahi ya bintiye kipaumbele kila wakati huku akimtakia maisha marefu na  baraka tele maishano.

"Malkia mwenyewe @keilah_oyando. Leo mniruhusu niringe na kifurushi changu cha furaha. Maneno hayawezi eleza jinsi alivyo mrembo. Maisha yangu yalibadilika punde ulipowasili. Maslahi yako yatakuwa ya kwanza kila wakati. Nakutakia maisha marefu na mafanikio. Asante @carrol_sonie kwa zawadi hii nzuri. Nawapenda nyote. Baraka." Mulamwah aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Kwa upande wake Sonnie alionekana kupendezwa na urembo wa bintiye huku akimhakikishia kwamba mapenzi aliyo nayo kwake ni makubwa sana.

Wapenzi hao wawili walitangaza kuzaliwa kwa kifungua mimba wao kupitia mitandao ya kijamii mnamo Septemba 20.

"Na ni msichana. Muujiza umewasili.. maneno hayaweza kueleza ninavyohisi, ni kitu cha maana zaidi kuwahi fanyika maishani mwangu. Karibu kipenzi @keilah_oyando" Mulamwah aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.