Itamgharimu Eric Omondi angalau ng'ombe 500 kuoa mshindi wa Wife Material, Monica Ayen

Muhtasari

•Mwanamitindo huyo kutoka nchi ya Sudan Kusini ameweka wazi kuwa mahari ambayo  atakayetazamia kumuoa anafaa kulipa ni angalau ng'ombe mia tano.

•Ayen ameeleza watu wao walio Juba hawakufurahishwa na kitendo chake na Omondi kubusu kabla ya kufunga ndoa na kufuatia hayo mcheshi huyo atahitajika kulipa faini ili kutuliza mashemeji.

• Omondi ameapa kwamba ako tayari kulipa mara tatu ya mahari ambayo mashemeji wake wanadai ili aweze kuoa kipenzi chake.

Image: INSTAGRAM

Itamgharimu mchekeshaji Eric Omondi mamilioni ya pesa kumuoa mshindi wa shoo ya Wife Material Monica Ayen.

Alipokuwa kwenye mahojiano na Mungai Eve, mwanamitindo huyo kutoka nchi ya Sudan Kusini ameweka wazi kuwa mahari ambayo  atakayetazamia kumuoa anafaa kulipa ni angalau ng'ombe mia tano.

"Mahari yangu ni ng'ombe mia tano. Kwetu tunatumia ng'ombe kulipa mahari. Hata hivyo unaweza tumia pesa kulipa lakini sisi ni wafugaji wa kuhama kwa hivyo tunafuga ng'ombe. Lazima ulipie hizo ng'ombe" Ayen alisema.

Mwanadada huyo ambaye ameyeyusha moyo wa Omondi amesema kuwa ako tayari kufunga ndoa na mcheshi huyo iwapo ako tayari kugharamia mahari yake yote.

Pia ameeleza watu wao walio Juba hawakufurahishwa na kitendo chake na Omondi kubusu kabla ya kufunga ndoa na kufuatia hayo mcheshi huyo atahitajika kulipa faini ili kutuliza mashemeji.

Kwa upande wake Omondi ameapa kwamba ako tayari kulipa mara tatu ya mahari ambayo mashemeji wake wanadai ili aweze kuoa kipenzi chake.

"Nitalipa. Nitawapatia ng'ombe 1,500, tutalipa faini. Nimeambiwa na watu wa Sudani Kusini kuwa nilichofanya ni dhambi na niko tayari kuomba msamaha. Lazima nilipe faini. Chochote watadai tutalipa mara tatu. Nitaenda na marafiki wangu sita kujadiliana na mashemeji. Sisi kutoka jamii ya Luo huwa tunajadiliana kuenda juu. Ukitaja bei tunakuambia ongeza" Omondi alisema.

Mcheshi huyo alisema kuwa atachukua hatua ya kuenda Sudani Kusini kulipa mahari ya Ayen hivi karibuni.