Harusi tunayo, hatuna? Eric Omondi afichua maafikiano yaliyofanywa katika mkutano wake na Jackie Maribe

Muhtasari

•Omondi ameeleza kuwa maafikiano ya mkutano wao hayakuwa kurudiana ila walipatana tu na kukubaliana kusuluhisha mzozo wao.

•Omondi amekiri kuwa walikosea kuhusisha mtoto kwenye malumbano yao huku akiapa kuwa sasa ako tayari kumwajibikia.

•Alisema kwamba matendo yao yenye aibu mitandaoni yalikuwa yamechangiwa sana na hasira kubwa iliyokuwa kwenye mioyo yao.

Jackie Maribe na Eric Omondi walipopatana siku ya Alhamisi
Jackie Maribe na Eric Omondi walipopatana siku ya Alhamisi
Image: SIMON KABU

Mcheshi Eric Omondi ameweka wazi yaliyojiri kati yake na Jackie Maribe walipopatana siku ya Alhamisi.

Akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz, msanii huyo asiyepungukiwa na drama za maisha alieleza kwamba waliletwa pamoja na mjasiriamali mashuhuri Simon Kabu kufuatia mzozo mkubwa uliokuwa unaendelea kati yao mitandaoni.

Omondi alieleza kwamba maafikiano ya mkutano huo hayakuwa kurudiana ila walipatana tu na kukubaliana kusuluhisha mzozo wao.

"Tulikuwa na mpatanishi ambaye ni Simon Kabu. Yeye ndiye alituleta pamoja..Hatujarudiana, tumekubaliana kuendelea mbele" Omondi alisema.

Licha ya kupatana kwao mchekeshaji huyo aliweka wazi kuwa hana mpango wa kufunga pingu za maisha na Bi. Maribe.

Omondi alikiri kwamba walikosea kuhusisha mtoto kwenye malumbano yao huku akiapa kuwa sasa ako tayari kumwajibikia.

"Mtoto ni mchanga, hajafanya chochote kibaya. Wazazi ndio wamekuwa wajinga, wamekosa kuwajibika, wamekuwa na utoto. Tumefanya maakosa. Lazima tuombe msamaha. Lazima turekebishe makosa yetu" Omondi alisema.

Alisema kwamba matendo yao yenye aibu mitandaoni yalikuwa yamechangiwa sana na hasira kubwa iliyokuwa kwenye mioyo yao.

Omondi amesema kuwa walishauriwa kujali hisia za mtoto wao na kuacha kumuweka kwenye hadharani wanapozozana.

Hata hivyo amesema kuwa kuna kitu kinachoendelea kuhusiana na drama zilizokuwepo kati yao na kueleza kuwa taarifa itatolewa hivi karibuni.

"Kwa sasa tumeshauriwa tuepuke jambo lolote linalohusisha mtoto kwa wiki chache tu. Kuna mambo tunapanga, tukimaliza tutatoa taarifa tukiwa pamoja" Omondi alisema.