Harmonize amuomba msamaha aliyekuwa mpenzi wake Sarah Michelloti, aeleza kilichovunja ndoa yao

Muhtasari

•Mmiliki huyo wa lebo ya Konde Music Worldwide alisema aliandika wimbo huo kuomba aliyekuwa mpenzi wake Sarah Michelloti msamaha kwa kuumiza moyo wake.

•Harmonize alisema ndoa yao ya miaka minne ilianza kusambaratika wakati mpenzi wake alikuwa amesafiri kuenda kwao na baada ya kuwa pweke kwa muda akapata majaribu ya kutembea na mwanadada aliyemzalia mtoto

•Harmonize alisema Sarah aliumia sana moyoni baada ya kupata habari kwamba mpenzi wake alikuwa amecheza karata nje na kupachika mwanadada mwingine ujauzito.

Harmonize na mpenzi wake Muitaliano Sarah Michelotti
Harmonize na mpenzi wake Muitaliano Sarah Michelotti
Image: HISANI

Hivi majuzi mwanamuziki Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize  alizindua albamu yake ya pili 'High  School'.

Staa huyo wa Bongo alitumia ukurasa wake wa Instagram kufafanulia mashabiki wake maana ya nyimbo ishirini zilizo kwenye albamu yake mpya.

Wimbo wa kwanza katika albamu ya Harmonize unaenda kwa jina 'Sorry'. (Pole)

Mmiliki huyo wa lebo ya Konde Music Worldwide alisema aliandika wimbo huo kuomba aliyekuwa mpenzi wake Sarah Michelloti msamaha kwa kuumiza moyo wake.

"Nyuma ya nyimbo zote kuna hadithi maalum. Wimbo wa kwanza 'Sorry' . NimeUweka nambari moja kwa sababu unaelezea hadithi za ukweli kuhusu tunayopitia maishani. Niliwahi chumbia mzungu. Kila mtu anamjua, Sarah. Yeye ndiye msukumo wa wimbo huo kwa sababu watu wengi tumekuwa tukianza mahusiano vizuri ila wakati yakawa si mazuri" Harmonize alisema.

Harmonize alisema ndoa yao ya miaka minne ilianza kusambaratika wakati mpenzi wake alikuwa amesafiri kuenda kwao na baada ya kuwa pweke kwa muda akapata majaribu ya kutembea na mwanadada aliyemzalia mtoto

"Ilikuja kipindi akawa anasafiri kuenda kwao. Nilikuwa Tanzania na kama unavyojua umbali wa mapenzi unapokuwa nikaishia kutembea na mwanamke ni mama Zuuh sasa hivi. Kwa mipango ya mwenyezi Mungu nikamfanya mjamzito. Akaniambia na kuniuliza ikiwa niko tayari ama atoe. Kwa kuwa mimi ni Muislamu, kuutoa mimba ni kushiriki  dhambi.  Sikuwa tayari kwa hayo. Niliamua ni njia ambayo mwenyez Mungu aliamua kunipitisha" Harmonize alisema.

Harmonize alisema Sarah aliumia sana moyoni baada ya kupata habari kwamba mpenzi wake alikuwa amecheza karata nje na kupachika mwanadada mwingine ujauzito.

Alisema alijaribu sana kumshawishi Sarah amsamehe ili warejeshe mahusiano yao ila juhudi zake zote ziliangulia patupu.

"Ilimuumiza sana Sarah kwa sababu mnapokuwa na mtu kwenye mahusiano mnakuwa na ndoto za kupata familia bora. Ilimuumiza sana na akashindwa kukubali. Kwa kipindi kirefu nilikuwa nikificha  almaradi tu mahusiano yetu yaweze kuenda vyema. Nilikuwa naamini ingawa alikuwa na hasira wakati ungefika akubali matokeo. Nilikuwa natafuta njia zingine za kuenda kwake ili awe sawa na yote lakini kwa bahati mbaya ilishindikana hakuweza kukubali na akaenda"  Harmonize alisimulia.

Staa huyo wa Bongo alisema kuzaliwa kwa mtoto huyo kuliibua mzozo mkubwa katika ndoa yao kwani walibishana kila siku kuhusu suala hilo. 

Alisema ilifikia wakati akaweka mapenzi yake kwa bintiye kabla ya yale aliyokuwa nayo kwa mkewe  na hapo ndipo wakatengana.

"Nilimwambia kama huo ndio mwisho wa mahusiano yetu ni sawa kwa sababu siwezi katupa damu yangu. Nilmwambia nataka kuwa baba mzuri. Ikafikia misuguano ya huku na kule mpaka mahusiano yetu ikaisha. Naamini Mungu alipanga tuwe pamoja kwa miaka minne." Konde Boy alisema.

Harmonize alisema baada ya muda yeye wote wawili waliweza kusonga mbele na kujitosa kwenye mahusiano mengine.

"Nashukuru kipindi cha miaka minne ambacho tulikuwa pamoja. Namshukuru na namtakia mazuri maishani" Alisema.

Harmonize alisema wimbo wake 'Sorry' unazungumzia hisia za kikweli kutoka moyoni mwake ila hakutazamia mahusiano yao yarejee.