"Imekuwa jehanamu kwangu lakini sasa niko tayari" Willy Paul ataja sababu za kunyamaza na kuchelewesha albamu yake

Muhtasari

•Nyota huyo wa muziki wa kisasa amesema amekuwa akipitia magumu siku za hivi karibuni na ndio maana akachelewesha albamu yake.

•Willy Paul anasema madai ya 'uongo' yaliyowasilishwa mahakamani dhidi yake yalikuwa karibu kuharibu kila kitu alichofanyia kazi kwa bidii ila Mungu sasa amemuonekania.

Image: INSTAGRAM// WILLY PAUL

Hatimaye albamu mpya ya mwanamuziki Wilson Radido almaarufu kama Willy Paul itaachiliwa wiki ijayo baada ya kusubiriwa kwa kipindi kirefu.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, nyota huyo wa muziki wa kisasa amesema amekuwa akipitia magumu siku za hivi karibuni na ndio maana akachelewesha albamu yake.

Willy Paul alikuwa anakusudia kuachilia albamu yake 'The African Experience' mnamo Oktoba 22 ila akatangaza sababu zisizozuilika zilimsukuma asitishe mpango huo.

Msanii huyo aliyezingirwa na utata mwingi katika taaluma yake ya muziki amesema alisimamisha mpango wa albamu yake ili kushughulikia kesi ambayo alishtakiwa kwa madai ya unyanyasaji wa kingono.

"Najua nimekuwa nimenyamaza lakini sasa nimerudi. Albamu #theafricanexperiencealbum itatoka wiki ijayo. Mungu amekuwa mwaminifu manze. Imekuwa jehanamu kwangu lakini sasa tuko tayari. Nililazimika kusimamisha albamu kwa sababu nilikuwa na kesi mahakamani" Willy Paul amesema.

Takriban miezi miwili iliyopita mwanamuziki Miss P alijitokeza kudai kuwa alipokuwa katika lebo ya Saldido Willy Paul alimnyanyasa kingono.

Miss P alisema Willy Paul alimnajisi mara kadhaa baada ya kuanza vikao vya studio pamoja naye.

"Yeye alinilazimisha kufanya ngono naye, si mara moja si mara mbili. Nilibidi kumwambia mama yangu kwa sababu nilipaswa kupata matibabu"Miss P alisema akiwa kwenye mahojiano.

Hata  hivyo Willy Paul amekuwa akikanusha madai ya Miss P huku akiyataja kuwa ya ya uongo, ya chuki na yenye nia ya kumharibia jina tu.

Wiki iliyopita mahakama ya Nairobi iliamuru Miss P aondoe video ambayo inaonyesha akitoa madai kuhusu Willy Paul kumnyanyasa kingono kutoka kwa mtandao wa youtube.

Willy Paul anasema madai ya 'uongo' yaliyowasilishwa mahakamani dhidi yake yalikuwa karibu kuharibu kila kitu alichofanyia kazi kwa bidii ila Mungu sasa amemuonekania.

"Mungu ni mwema. Tumerudi kana kwamba hatukuenda mahali. Hivi karibuni nitasema kila kitu. Lakini kabla ya albamu niko na kitu maalum kwenu, maalum sana" Willy Paul amesema.