"Hatukuoana ili tuachane!" Mamake Diamond, Mama Dangote na mpenziwe wapuuzilia mbali madai kuwa wametangana

Muhtasari

•Wawili hao wameweka wazi kuwa wangali pamoja na hamna msukosuko wowote katika ndoa yao ya miaka mitano.

•Shamte alisema hatua yake ya kusafiri na kukosekana nyumbani kwao ndiyo ilisababisha uvumi kuhusu kutengana kwao.

•Wanandoa hao waliwasuta vibaya walimwengu wanaotakia ndoa yao mabaya huku akidai vitendo vyao ni vya kusikitisha sana.

Diamond, Uncle Shamte, Mama Dangote
Diamond, Uncle Shamte, Mama Dangote
Image: INSTAGRAM

Mama Dangote ambaye ni mama ya staa wa Bongo Diamond Platnumz pamoja na mume wake Rally Jones almaarufu kama Uncle Shamte wamepuuzilia mbali madai kuwa ndoa yao imesambaratika.

Walipokuwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, wawili hao waliweka wazi kuwa wangali pamoja na hamna msukosuko wowote katika ndoa yao ya miaka mitano.

Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita uvumi umekuwa ukitanda kote Bongo kuwa kitumbua kimeingia mchanga baada ya wanandoa hao wawili kutoonekana pamoja kwa muda. Hata hivyo wapenzi hao wametoa hakikisho kuwa ndoa yao ingali imara.

"Kuachana iweje. Sisi wenyewe ni Waislamu na kwetu talaka ni dhambi. Sio kitu kizuri. Sio kitu cha kushabikia wala kuongelea ama kushauri mtu ampe  mwenzake talaka. Sisi hatuko huko" Uncle Shamte alisema.

Shamte alisema hatua yake ya kusafiri na kukosekana nyumbani kwao ndiyo ilisababisha uvumi kuhusu kutengana kwao.

Alisema walifanya maamuzi ya kufunga  ndoa ndiposa waishi pamoja kwa raha huku akisisitiza kuwa ni jukumu lake kumlinda mamake Diamond.

"Nilisafiri. Mimi nimesafiri, sionekani. Kuachana ndio nini? Sisi hatujaoana kwa ajili ya kuachana. Tumeoana kwa ajili ya kuishi. Mimi ndio nina kazi kubwa ya kumlea mama yenu. Naomba hilo neno mlibadilishe" Alisema Shamte.

Wanandoa hao waliwasuta vibaya walimwengu wanaotakia ndoa yao mabaya huku akidai vitendo vyao ni vya kusikitisha sana.

Wawili hao walijitosa kwenye mahusiano zaidi ya miaka mitano iliyopita na wameendelea kuweka mahusiano yao wazi tangu wakati huo.