Size 8 aunga mkono muswada wa Eric Omondi unaopendekeza kukuzwa kwa muziki wa Kenya

Muhtasari

•Amesema ukuzaji wa sekta ya muziki hapa nchini utakuwa wa msaada mkubwa haswa kwa kizazi kipya ikiwemo watoto wake iwapo wataamua kujitosa katika muziki.

Image: INSTAGRAM// SIZE 8

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Linet Munyali almaarufu kama Size 8 ameunga mkono muswada unaosukumwa na Eric Omondi ambao unapendekeza vituo na maeneo ya burudani nchini kucheza 75% ya muziki wa hapa Kenya.

Alipokuwa anazungumza na wanahabari siku ya Jumapili, Size 8 alisema angependa muswada huo upitishwe kwani vituo vya burudani hapa nchini hupendelea sana kucheza muziki wa kimataifa.

Mke huyo wa mcheza santuri DJ Moh amesema ukuzaji wa sekta ya muziki hapa nchini utakuwa wa msaada mkubwa haswa kwa kizazi kipya ikiwemo watoto wake iwapo wataamua kujitosa katika muziki.

"Hatuwezi kataa hiyo kwa sababu Kenya ni mojawapo wa nchi chache ambapo muziki unaochezwa kwa redio sanasana si wa hapa nchini. Ukienda Uganda, 90% ya muziki unaochezwa ni wa pale, ukienda Afrika Kusini, Nigeria na Tanzania wanacheza  90% ya muziki wa pale. Hatuungi muswada huu mkono kwa ajili yetu binafsi, hata watoto wetu kina Ladasha wakitaka kuimba atasaidika. Acha tukuze muziki kwa sababu kuna wasanii wengi chipukizi" Alisema Size 8.

Mwanamuziki huyo alishawishi vyombo vya habari kucheza muziki wa Kenya zaidi huku akisema angependekeza vicheze asilimia 90%.