"Hatujazungumza miaka miwili!" Mkewe Mr Seed afunguka kuhusu uhusiano wake na Diana Marua

Muhtasari

•Nimo  alifichua hakujakuwa na mawasiliano yoyote kati yake na Diana kwa kipindi cha takriban miaka miwili iliyopita wala kukutana ana kwa ana.

•Alisema alikosa kuhudhuria hafla ya kuzindua Diana kama mwanamuziki kwa kuwa mwaliko ulikuja kuchelewa na tayari alikuwa na mipango mingine.

Diana Marua na Nimo Gachuiri
Diana Marua na Nimo Gachuiri
Image: HISANI

Bi Nimo Gachuiri ambaye ni mke wa mwanamuziki  mashuhuri Mr Seed hatimaye amemwaya mtama kuhusu uhusiano wake wa sasa  na mke wa Bahati Diana Marua. 

Alipokuwa kwenye mahojiano na Nicholas Kioko, Nimo aliweka wazi kwamba hana ugomvi wowote na rapa huyo chipukizi. 

Nimo  hata hivyo alifichua hakujakuwa na mawasiliano yoyote kati yake na Diana kwa kipindi cha takriban miaka miwili iliyopita wala kukutana ana kwa ana.

"Kusema kweli hatujazungumza na Diana kwa kipindi cha miaka miwili sasa. Hatujawahi kuongea, hatujawahi kutana ana kwa ana. Mimi sina ugomvi na yeye. Nahisi hakuna haja ya kuzozania mambo yaliyotendeka miaka miwili iliyopita. Ni ufala." Nimo alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema ingawa hajawahi kupiga hatua ya kumfikia Diana ili wasuluhishe mzozo wao, tayari amekubali kusahau yaliyopita.

Alisema alikosa kuhudhuria hafla ya kuzindua Diana kama mwanamuziki kwa kuwa mwaliko ulikuja kuchelewa na tayari alikuwa na mipango mingine. Hata hivyo alisema alifuatia hafla hiyo.

"Nilikuwa nimealikwa. Baha alianiambia Jumapili. Nilikuwa na mipango mingine  siku hiyo. Nilikuwa nahudhuria hafla ya kanisa. Kulikuwa na dress code na unajua sisi wanawake hatuwezi kutokea hivo tu. Nilifuatilia lakini nyuma ya pazia" Nimo alisema.

Nimo alisema hatua ya Diana kujitosa kwenye muziki ni nzuri huku akimhimiza asikufe moyo kutokana na chuki dhidiyake mitandaoni.