"Mimi si homebreaker!" Karen Nyamu azungumzia uhusiano wake na Samidoh pamoja na mkewe

Muhtasari

•Nyamu alipuuzilia mbali madai kuwa ana nia ya kuvunja ndoa ya Samidoh na kuweka wazi kwamba hana nia yoyote mbaya dhidi ya mwanamuziki huyo wala familia yake.

•Nyamu alisema anamheshimu sana mke wa mwanamuziki huyo na hashindani naye kwani anaelewa vyema kamwe hawezi kujaza nafasi yake katika maisha ya Samidoh.

Samidoh na Karen Nyamu
Samidoh na Karen Nyamu
Image: INSTAGRAM

Wakili na mwanasiasa Karen Nyamu amefunguka kuhusu uhusiano wake na nyota wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu kama Samidoh.

Akiwa kwenye mahojiano na Mungai Eve, mgombeaji huyo wa kiti cha useneta kaunti ya Nairobi mwaka ujao alisema kwa sasa yeye na mwanamuziki huyo ni marafiki wakubwa.

Nyamu alipuuzilia mbali madai kuwa ana nia ya kuvunja ndoa ya Samidoh na kuweka wazi kwamba hana nia yoyote mbaya dhidi ya mwanamuziki huyo wala familia yake.

"Najua sitaki kuharibu. Najua mimi sio mtu wa kuvunja boma. Najua nia yangu si mbaya. Najua sio kitu kizuri lakini ni hali ambayo tulijipata. Mimi  na Samidoh ni marafiki wakubwa,tuko na mtoto tunayependa sana ambaye  tunalea. Sisi ni marafiki wakubwa na tunasaidiana" Nyamu alisema.

Mama huyo wa watoto wawili pia alikana madai ya kujaribu kumkomoa mke wa Samidoh kupitia matendo yake ya mitandaoni.

Nyamu alisema anamheshimu sana mke wa mwanamuziki huyo na hashindani naye kwani anaelewa vyema kamwe hawezi kujaza nafasi yake katika maisha ya Samidoh.

"Hana lolote kuhusiana na maamuzi yangu. Hatuko kwenye mashindano. Huwezi shindana na mtu ambaye huwezi kachukua nafasi yake. Huyo ni mke wa kwanza, huyo ni mama yao. Siwezi kachukua nafasi yake kwa sababu amejenga boma. Huyo ni mwanamke ninayemkubali, najua siwezi jaza nafasi yake. Namheshimu, namkubali kama mama na kama mke. Sina chochote dhidi yake" Alisema.

Nyamu ambaye anatarajia mtoto mwingine na mwanamuziki huyo pia alikiri hakuwa amepangia ujauzito anaoubeba kwa sasa ila akasema hana majuto yoyote.