"Tuna muda mrefu hatujawasiliana!" Mbosso azungumza kuhusu ugomvi wake na Aslay

Muhtasari

•Mbosso alithibitisha kutofautiana kwake na mwanamuziki Aslay Isihaka Nassoro (Aslay) huku akiweka wazi kwamba hawajawasiliana kwa kipindi kirefu.

•Mbosso alisema juhudi zake za kumpata Alsay ziligonga mwamba kwani alishindwa kuafikiana na mameneja wake ambao alikuwa anawasiliana nao.

Mbosso na Aslay
Mbosso na Aslay
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki mashuhuri kutoka Tanzania Mbwana Yusuf Kilungi almaarufu kama Mbosso amefunguka  kuhusu uhusiano wake na wasanii waliokuwa wenzake katika bendi ya Yamoto.

Akiwa kwenye mahojiano na wanahabari jijini Mombasa, Mbosso aliweka wazi kwamba bado huwa anawasiliana mara kwa mara na Enock Bella pamoja na Beka Flavour.

Mbosso hata hivyo alithibitisha kutofautiana kwake na mwanamuziki Aslay Isihaka Nassoro (Aslay) huku akiweka wazi kwamba hawajawasiliana kwa kipindi kirefu.

"Huwa tunazungumza zaidi na Enock Bella, Beka Flavour nawasiliana naye, Aslay tuna muda mrefu kidogo hatujawasiliana ila tunawasiliana. Nikisema hatuwasiliani ni uwongo, ila  tunawasiliana tu" Mbosso alisema.

Nyota huyo wa Bongo alisema alipokuwa anatayarisha albamu yake alifanya jitihada za kuwatafuta wanabendi wenzake wa zamani ili wafanye muziki pamoja na akafanikiwa kuwapata Enock na Beka.

Mbosso alisema juhudi zake za kumpata Alsay ziligonga mwamba kwani alishindwa kuafikiana na mameneja wake ambao alikuwa anawasiliana nao.

"Kipindi naandaa albamu yangu nilimcheki Enock, nikamcheki Beka, nikamcheki Aslay kupitia uongozi wake. Kwa wawili iliwezekana, kumpata Enock na Beka iliwezekana ila kwa upande wa uongozi wa Aslay kidogo kulikuwa na uzito. Sikuweza kuilazimisha sana kwa sababu nafahamu hii ni biashara na kila mtu ana mikataba yake. Nilikuwa nawasiliana na meneja wake anaitwa Chambuso ambaye pia alikuwa meneja wetu Yamoto band. Aliniambia kwa wakati huo jambo hilo lilikuwa ngumu. Nilimwambia  sawa kama haiwezekani hamna tatizo, ila kwa sababu niko katika kupangilia uzinduzi nitawapa mwaliko. Niliwaomba waje kwenye uzinduzi. Waliitikia kuwa kwenye uzinduzi lakini nilishindwa kuufanya kwa sababu tulipatwa na msiba mkubwa sana. Tulipokuwa tunakaribia kufanya uzinduzi ndipo alitekuwa rais wetu mheshimiwa Magufuli akawa amefariki kwa hivyo sikuweza kufanya kitu" Mbosso alisema.

Staa huyo alisema hangeweza kuendelea kufanya wimbo na wanabendi wenzake wa kitambo kama alivyotaka kwani lengo lake lililuwa afanye na wote watatu pamoja.

Mbosso alisema angependa kufanya muziki pamoja na watatu hao siku zijazo huku akiwahakikishia kwamba angali anawapenda kama ndugu zake.