"Mama ana furaha!" Mtangazaji Gidi aandaa karamu ya kufana kusherehekea kustaafu kwa mama yake

Muhtasari

•Marafiki wa karibu na wanafamilia ni miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ya kutoa shukrani kufuatia kustaafu kwa Bi Oyoo ambaye amekuwa akihudumu kama mwalimu kwa kipindi cha zaidi ya miongo minne

Marafiki wahudhuria hafla ya kusherehekea kustaafu kwa mama yake Gidi
Marafiki wahudhuria hafla ya kusherehekea kustaafu kwa mama yake Gidi
Image: INSTAGRAM// GIDI OGIDI

Siku ya Jumatatu mtangazaji wa kipindi cha 'Gidi na Ghost asubuhi' Gidi Ogidi aliandaa karamu ya kufana kijijini kwao Homabay kusherehekea kustaafu kwa mama yake, Mama Oyoo.

Marafiki wa karibu na wanafamilia ni miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ya kutoa shukrani kufuatia kustaafu kwa Bi Oyoo ambaye amekuwa akihudumu kama mwalimu kwa kipindi cha zaidi ya miongo minne.

Gidi alitumia ukurasa wake wa Instagram kuwashukuru marafiki waliofanikisha siku hiyo maalum kwa mamake.

"Asante marafiki.. mama ana furaha!" Gidi aliandika.

Baadhi ya marafiki waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na mtangazaji wake mwenza Ghost Mulee, mchekeshaji Jalang'o, kocha wa zamani wa Harambee Stars Adel Amrouche, mwanaharakati Brian Weke kati ya wengine wengi.

Gidi alijivunia hafla hiyo maridadi iliyokuwa imepambwa kweli huku akiwashukuru sana marafiki wake kwa kumfanya mama yake mwenye raha.

Wiki iliyopita Gidi alifichua mpango wake wa kuandaa hafla ya kumshukuru Mola kwa huduma ambayo mama yake alitoa kwa kipindi cha ya miaka 41.

"Ikiwa uliwahi kufundishwa na Bi Oyoo, amestaafu rasmi taaluma ya ualimu baada ya miaka 41 ya utumishi. Tunakusudia kumsherehekea wiki ijayo katika hafla ya kushiriki maombi ya shukrani pale nyumbani kwake. Wanafunzi wote wa zamani na marafiki ambao wangependa kupitisha ujumbe wa shukrani kumpa zawadi Mwalimu tafadhali wasiliana na Dk @mark_ojuok au nitumie ujumbe. Hongera sana Mama kwa kustaafu" Gidi aliandika.

Kutoka Radio Jambo tunamtakia Mama Oyoo kustaafu kuzuri.