"Nilishtuka!" Karen Nyamu afunguka kuhusu alivyopokea habari za ujauzito wake wa pili Samidoh

Muhtasari

• Karen alisema aligundua hali yake wakati alikuwa anafanya utafiti kubaini ni kiti kipi bora kuwania Nairobi pamoja na kufanya maandalizi ya kampeni zake.

•Alisema mzazi wake mwenza, Samidoh pia alipokea habari zile kwa furaha kubwa huku akiweka wazi kwamba nyota huyo wa Mugithi anapenda watoto sana.

Karen Nyamu na Samidoh
Karen Nyamu na Samidoh
Image: HISANI

Wakili na mwanasiasa mashuhuri nchini Karen Nyamu amekiri kwamba alishtuka alipopata habari kuhusu ujauzito wake wa tatu ambao ameubeba kwa sasa.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Karen alisema aligundua hali yake wakati alikuwa anafanya utafiti kubaini ni kiti kipi bora kuwania Nairobi pamoja na kufanya maandalizi ya kampeni zake.

Nyamu ambaye anatarajia mtoto wake wa pili na mwanamuziki Samuel Muchoki almaarufu kama Samidoh alisema alipopata habari zile hakujua jinsi ya kuzichukulia ila baadae akawa anazifurahia. Alisema anasubiri sana kumkumbatia mtoto aliyebeba tumboni mwake.

"Nilipopata habari kuhusu ujauzito wangu, sikujua jinsi ya kuzichukulia kwani nilikuwa najiandaa kwa kampeni. Tulikuwa tunafanya utafiti kuhusu nafasi ipi bora yangu kuwania Nairobi.  Nilipopata habari nilishtuka kiasi, sikujua jini ya kupokea  habari hizo. Lakini hatimaye nilifurahi sana kwa sababu ujauzito ni wakati wa kusisimua kwa mama yeyote. Nina furaha sana, nimefurahi, siwezi kusubiri kukutana na mtoto wangu mdogo" Bi Nyamu alisema.

Wakili huyo alisema mzazi wake mwenza, Samidoh  pia alipokea habari zile kwa furaha kubwa huku akiweka wazi kwamba nyota huyo wa Mugithi anapenda watoto sana.

Bi Nyamu pia alisema kifungua mimba wake anafurahi sana kujua kwamba hivi karibuni atakuwa na ndugu.

"Yeye ndiye aliyefurahi zaidi. Anabusu tumbo yangu kila wakati anapokaribia kuondoka kwa nyumba kuenda shule. Akirudi nyumbani pia ananibusu tumboni. Anampenda kakake mdogo. Nadhani yeye ndiye mwenye furaha zaidi" Alisema.

Tayari mwanasiasa huyo ana mtoto mmoja wa kiume na Samidoh. Sam Juniour alihitimu mwaka mmoja mwezi uliopita.