Je, kuna mahusiano ya kimapenzi kati ya Zuchu na Diamond? - Khadija Kopa apasua mbarika

Muhtasari

•Hii ni kufuatia uvumi unaoenezwa kuwa nyota hao wawili wa Bongo wanachumbiana baada yao kuonekana hotelini pamoja siku ya Krismasi.

Diamond Platnumz, Khadija Kopa, Zuchu
Diamond Platnumz, Khadija Kopa, Zuchu
Image: HISANI

Mtunzi na mwimbaji  mashuhur wa nyimbo za taarabu kutoka Zanzibar Khadija Omar Kopa  amepasua mbarika kuhusu uhusiano wa bintiye  Zuhura Othman Soud almaarufu kama Zuchu na bosi wa WCB Diamond Platnumz.

Hii ni kufuatia uvumi unaoenezwa kuwa nyota hao wawili wa Bongo wanachumbiana baada yao kuonekana hotelini pamoja siku ya Krismasi.

Alipokuwa kwenye mahojiano na Mbengo TV, Bi Kopa alipuuzilia mbali madai hayo huku akisema alishtuka sana uvumi kuhusu mahusiano ya bintiye na Diamond ulipovumishwa mitandaoni.

Kopa alisema bintiye aliwasiliana na bintiye na akamueleza hali halisi kuwa huo ni uvumi tu usio na msingi. Zuchu alimhakikishia mamake kuwa Diamond amekuwa akionyesha heshima kubwa kwake na hakuna chochote kinachoendelea kati yao.

"Wakati ule Zuhura aliniambia Diamond anamheshimu sana na hajawahi hata siku  moja kuniambia vitu vya kipuzi. Nilishtuka maanake watu walikuwa wanavumisha kupita kiasi. Nilishangaa mbona walivumisha kupita kiasi. Mimi mwenyewe sikushughulika sana. Nilimuuliza Zuhura mbona watu walivumisha sana ama kuna kitu chochote. Aliniambia hamna wala hajawahi kuvunjiwa heshima hata siku moja. Mimi nilichukulia kama kitu cha kawaida" Alisema Khadija Kopa.

Bi Kopa aliweka wazi kuwa kwa miaka mingi Diamond anamchukulia kama mamake na amekuwa akimheshimu sana.

Alisema kwamba  yeye ndiye aliyempeleka Zuchu Wasafi na wakati ule Diamond alimchukulia binti yake kama mdogo wake.

"Diamond mimi ananiona kama mamake kusema ukweli. Tangu zamani, kabla ata huyo Zuchu  hajaenda Wasafi, amenichukulia kama mamake. Siku niliyomwelekeza mwanangu ata kabla aende WCB nilimwambia wewe ndio meneja wangu. Alimchukulia kama mdogo wake, hamtanii" Alisema Kopa.

Gwiji huyo wa Taarab alisema Diamond alishangaa wakati alipokabidhiwa Zuchu WCB kwani alimuona kama mwanadada mpole sana.

Alisema kwamba binti yake aliwahi kumtambulisha mwanamume mmoja tu kama mpenzi wake ila mahusiano yao hayakudumu.