Madaktari waliwahi kumtabiria kifo baada ya mwaka mmoja- Churchill azungumzia ugonjwa wa Akuku Danger

Muhtasari

•Churchill alifahamisha waliohudhuria kwamba Akuku Danger alizaliwa na maradhi hatari ya saratani ya damu (Sickle Cell Anemia) .

•Umati uliokuwa umehudhuria shoo hiyo uliweza kuchanga shilingi laki nne katika kipindi cha dakika tatu pekee.  

Daniel Ndambuki, Akuku Danger
Daniel Ndambuki, Akuku Danger
Image: INSTAGRAM

Mnamo mkesha wa mwaka mpya mchekeshaji maarufu Daniel 'Churchill' Ndambuki alifanya shoo yake ya Churchill Show maalum kwa mchekeshaji wake Akuku Danger ambaye anaugua.

Katika shoo hiyo iliyofanyika Garden City , Churchill aliwaeleza mashabiki machache kuhusu ugonjwa ambao Akuku Danger amekuwa akipambana nao kabla ya kuwaomba wasaidie kuchanga pesa za kugharamia matibabu yake ghali.

Churchill alifahamisha waliohudhuria kwamba Akuku Danger alizaliwa na maradhi hatari ya saratani ya damu (Sickle Cell Anemia) . Alifichua kwamba mchekeshaji huyo wake amekuwa akilazwa hospitalini mara kwa mara na hata  kuambiwa amebakiza muda gani wa kuishi.

"Tulienda kumuona katika hospitali ya Nairobi West na Akuku Danger alizaliwa na saratani ya damu. Huwa inakuja mara kwa mara kisha inaenda. Yeye huwa analazwa mara kwa mara. Kusema kweli kitu kimoja ambacho kimemweka hai ni yeye kuweza kuja hapa na kuwaburudisha. Hilo limemfanya kuendelea licha ya madaktari kumwambia ana mwaka mmoja na miezi wa kuishi" Churchill alisema.

"Je wajua hilo lamaanisha nini? Daktari anakwambia una miezi sita ya kuishi kisha unamaliza mwaka? Anakwambia sasa uko na mwaka mwingine mmoja!" Aliendelea kusema

Aliwaeleza waliohudhuria kwamba mwathiriwa wa ugonjwa huo hatari anapopata nafuu kisha baadae ugonjwa unashambulia tena huwa unarejea na nguvu zaidi na kulemea mgonjwa zaidi.

Umati uliokuwa umehudhuria shoo hiyo uliweza kuchanga shilingi laki nne katika kipindi cha dakika tatu pekee.