Mapenzi yashinda! Guardian Angel na mpenziwe Esther Musila wafunga pingu za maisha

Muhtasari

•Wawili hao walifanya harusi ya faragha iliyohudhuriwa na wanafamilia na marafiki wachache mnamo Jumanne  tarehe 4  mwezi Januari, 2022

•Bi Musila alisherehekea hatua waliyopiga na mpenzi wake huku akimtaja mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 31 kama mtu maalum na rafiki wake wa dhati.

Guardian Angel, Esther Musila
Guardian Angel, Esther Musila
Image: INSTAGRAM

Hatimaye mwanamuziki wa nyimbo za injili Peter Omwaka almaarufu kama Guardian Angel na mpenzi wake Esther Musila  wamefunga ndoa rasmi.

Wawili hao walifanya harusi ya faragha iliyohudhuriwa na wanafamilia na marafiki wachache mnamo Jumanne  tarehe 4  mwezi Januari, 2022

Guardian Angel na Bi Musila walitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kufahamisha walimwengu kuhusu hatua hiyo muhimu ambayo walipiga.

"Na katika siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwangu, Mungu alinitendea tena. Bw na Bi Omwaka... mke wangu @esther.musila" Guardian Angel alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Bi Musila alisherehekea hatua waliyopiga na mpenzi wake huku akimtaja mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 31 kama mtu maalum na rafiki wake wa dhati.

Kwenye chapisho lake Instagram, Malkia huyo mwenye umri wa miaka 51 alikiri kamwe maishani hakuwahi kufikiria kwamba angepatana na mpenzi kama Guardian Angel.

"Kupata mtu maalum kama wewe kati ya watu wote ulimwenguni ni jambo ambalo sikuwahi kufikiria. Wacha tufanye maisha haya pamoja. Bw na Bi Omwaka" Esther aliandika.

Wanandoa hao wawili wamekuwa katika mahusiano kwa kipindi cha takriban miaka miwili na  wamekuwa wakijivunia maamuzi waliyofanya ya kuwa pamoja licha ya ukosoaji mkubwa ambao wamekabiliana nao  kufuatia pengo kubwa kati ya umri wao.

Esther ana watoto wawili wakubwa kutoka kwa ndoa yake ya hapo awali. Aliyekuwa mume wake na ambaye ni baba ya watoto wake watatu aliaga dunia takriban miaka mitano iliyopita.